LONGIDO: Fedha Sh milioni 90 zimechangwa ili kuvuta maji kutoka chanzo cha maji kilichopo kata ya Sinonik, Wilaya ya Longido kwa lengo la kuwahakikishia wananchi wa kata hiyo maji safi na salama.
Kiasi hicho cha fedha kitawezesha pia mabomba, ujenzi wa tanki lita 100,000 na ujenzi eneo la maji ya mifugo.

Fedha hizo zimechangwa na Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, wananchi wa kata hiyo na shirika lisilo la kiserikali la Pingo’s Forum.
Dk Kiruswa pekee alinunua mabomba ya maji ya Sh milioni 18, na wananchi milioni 2, ili kusambaza maji maeneo ya vijijini umbali wa km 4.

Akizungumza leo Desemba 25, Dk Kiruswa amesema chanzo hiko cha maji ni muhimu, hivyo aliwaomba wananchi kulinda miundombinu yake kwa gharama kubwa.
Amesema chanzo hiko kilichopo mpakani mwa Kenya kilikuwa kikitumiwa na wananchi wa taifa hilo, baada ya kutandaza mabomba ya maji toka chanzo hicho, hali hiyo iliwafanya wananchi wa Sinonik kupata changamoto ya maji.
Dk Kiruswa amewataka wananchi kujitoa katika miradi midogo midogo kwa hali na mali kama vile maji na miradi mingine na kusema kuwa serikali itakuwa ikitoa fedha kwa miradi mikubwa yenye tija kwa jamii na kazi ya kuchimba ili bomba ziweze kupita ni shughuli zinazopaswa kufanywa na wananchi na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiona juhudi za wananchi itajitoa zaidi.
Amesema na kuwataka wananchi kujitoa kuhakikisha mradi huo wa maji unaisha mwaka huu ili aweze kwenda kufungua ili wananchi wasihangaike kusaka maji nyakati za usiku na alfajili kwani ni hatari kutokana na kata ya Sinonik kuwa na wanyama wakali.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Longido mkoani Arusha, Thomas Ngobei aliwataka viongozi wa vijiji katika halmashauri hiyo kuwashirikisha wataalamu wa maji lengo ni kutaka ujenzi wa tanki,ujenzi wa chanzo cha maji na eneo la maji kwa ajili ya mifugo unajengwa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na wataalamu hao.

Aidha, aliwapongeza Pingo’s Forum kwa kujitoa kwa hali na mali katika ujenzi wa mradi wa maji kata ya Sinonik na kusema kuwa jitihada hizo zinapaswa kupongezwa na kuyataka mashirika mengine kuiga mfano wa Shirika hilo lenye nia njema kwa wananchi wa Longido na kuacha kufanya kazi isiyikusudiwa katika wilaya hiyo.
Naye Mratibu wa Mradi wa Kuimarisha Huduma kwa Jamii Pembezoni mwa Wilaya ya Longido wa Shirika la Pingo’s Forum, Kiaro Tendeu amesema mradi huo uliopo kijiji cha Kimwati kata ya Sininik amesema kuwa hadi sasa mradi huo umegharimu zaidi ya Sh milioni 70 ikiwemo ujenzi wa tank, ujenzi wa eneo la kunywa maji mifugo na eneo la chanzo cha maji, wananchi Sh milioni 2 na wanataka kabla ya desemba 31 mwaka mradi huo uwe umekamilika.
Tendeu amesema lengo la Pingo’s Forum katika wilaya ya Longido ni kutaka huduma muhimu kwa wananchi wa wilaya hiyo kama vile maji,elimu,afya na barabara zinawafikia mbali ya serikali kutoa msaada wa mamilioni ya fedha ila na wao watachangia kiasi fulani katika maeneo ya pembezoni ili kila mmoja afurahie matunda ya serikali iliyopo madarakani.
Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha Kimwati kwanza alimshukuru Mbunge kwa msaada wa mabomba ya maji na kusema moyo wa kujitoa wa Kiruswa unapaswa kupongezwa kwa dhati na pia aliwashukuru Pingo’s Forum msaada wa ujenzi wa tank,eno la chanzo cha maji na mifugo na kuwaahidi kuwa watakuwa walinzi wa mradi huo mchana na usiku.