Mkuu wa Wafanyakazi wa Serikali ya Libya ya Jeshi la Umoja wa Kitaifa, Luteni Jenerali Mohammed Al-Haddad, Oktoba 2018

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Mkuu wa Majeshi ya Libya anayehusishwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Luteni Jenerali Mohammed Al-Haddad, alifariki Jumanne, Desemba 23, 2025, pamoja na watu wanne waliokuwa wakisafiri naye. Ajali hiyo ilitokea baada ya mawasiliano kupotea na ndege yao muda mfupi baada ya kuondoka mjini Ankara, Uturuki, walipokuwa wakirejea Libya kutoka safari rasmi, kulingana na Shirika la Habari la Libya.

Kwa mujibu wa Makao Makuu ya Jeshi la Libya, waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu, Luteni Jenerali Al-Fitouri Ghraibil, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uzalishaji wa Kijeshi, Brigedia Jenerali Mahmoud Al-Qatawi, na mshauri wa Mkuu wa Majeshi, Muhammad Al-Asawi Diab.

Tukio hili limekumbusha ajali nyingine kubwa za anga zilizowaua viongozi wa kisiasa na kijeshi duniani.

Ajali ya Rais wa Iran, Ebrahim Raisi

Ubalozi wa Iran mjini Moscow, Russia, uliweka picha ya Rais wa Iran Ebrahim Raisi mbele ya jengo lake baada ya helikopta iliyokuwa imembeba kuanguka karibu na mpaka wa Irani na Azerbaijan, Mei 20, 2024.

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, alifariki tarehe 19 Mei 2024 katika ajali ya helikopta katika jimbo la Azerbaijan Mashariki, karibu na mpaka wa Azerbaijan. Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo, Hossein Amir-Abdollahian, pamoja na maafisa wengine wakuu, pia walifariki.

Raisi alikuwa ametembelea eneo hilo kwa ajili ya kuzindua bwawa la “Qiz Qala Si” pamoja na Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev. Helikopta ilipata ajali ilipokuwa ikirejea mjini Tabriz na kuanguka katika misitu ya Dezmar. Uchunguzi wa jeshi la Iran ulisema ajali ilisababishwa na ukungu mzito, ingawa madai ya hitilafu za kiufundi yaliibua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi.

Kifo cha kamanda wa Wagner, Yevgeny Prigozhin

Ukumbusho wa muda wa Yevgeny Prigozhin ulijengwa huko St. Petersburg, mahali alipozaliwa nchini Urusi, siku 40 baada ya kifo chake.

Chanzo cha picha, Reuters

Yevgeny Prigozhin, kamanda wa kundi la wanamgambo la Wagner, alifariki Agosti 2023 katika ajali ya ndege kaskazini-magharibi mwa Moscow, pamoja na watu wengine kumi. Kifo chake kilizua mjadala mkubwa, kwani kilitokea miezi miwili baada ya kuongoza uasi dhidi ya jeshi la Urusi.

Ingawa hakuwa na wadhifa rasmi serikalini, Prigozhin alikuwa na ushawishi mkubwa. Alijulikana kama “mpishi wa Putin” kutokana na biashara zake za awali, kabla ya kupanua shughuli zake hadi mikataba mikubwa ya kijeshi kupitia kundi la Wagner.

Rais wa zamani wa Pakistan, Muhammad Zia-ul-Haq

Rais wa Pakistani Muhammad Zia-ul-Haq, kwenye Uwanja wa Ndege wa Heathrow mjini London, Oktoba 1980

Rais wa zamani wa Pakistan, Muhammad Zia-ul-Haq, alifariki Agosti 1988 baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kulipuka karibu na mji wa Bahawalpur. Maafisa wakuu wa jeshi walikuwa naye ndani ya ndege hiyo.

Kwa miaka mingi, kifo chake kimekuwa kikihusishwa na nadharia mbalimbali, zikiwemo madai kuwa ndege ilishambuliwa kwa kombora au kulikuwa na vilipuzi vilivyofichwa ndani ya mizigo.

Malkia Alia wa Jordan

Malkia Alia wa Jordan kwenye Uwanja wa Ndege wa Heathrow huko London, Septemba 1973

Chanzo cha picha, Getty Images

Malkia Alia Al-Hussein, mke wa marehemu Mfalme Hussein bin Talal wa Jordan, alifariki Februari 1977 katika ajali ya helikopta alipokuwa akirejea kutoka ziara ya kikazi kusini mwa Jordan. Waziri wa Afya wa Jordan na wajumbe wengine pia walifariki.

Baada ya kifo chake, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amman ulipewa jina lake kwa heshima yake.

Rais wa zamani wa Iraq, Abdul Salam Arif

Rais wa Iraq Abdul Salam Arif (kushoto), akiwa amesimama na kikundi kwenye Hoteli ya Baghdad baada ya mkutano na waandishi wa habari, Januari 1963.

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais wa zamani wa Iraq, Abdul Salam Arif, alifariki Aprili 1966 akiwa na umri wa miaka 45 katika ajali ya helikopta karibu na mji wa Basra. Alikuwa katika ziara ya kikazi akiwa na mawaziri na wasaidizi wake, ambao wote walifariki katika ajali hiyo.

Baada ya kifo chake, alirithiwa na ndugu yake Abdul Rahman Arif, aliyelitawala taifa hilo kwa kipindi cha miaka miwili.

Jenerali Francis Ogolla & Viongozi wengine wa kijeshi

Ogolla aliteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi katika mabadiliko katika jeshi la Kenya mnamo Aprili 2023.

Chanzo cha picha, KDF

Nchini Kenya, Mkuu wa Majeshi wa Kenya, Jenerali Francis Ogolla, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa kijeshi na viongozi, walifariki dunia katika ajali ya helikopta katika eneo la Elgeyo-Marakwet MnamoAprili 2024.

Watu wengine waliofariki ni pamoja na Maafisa wakuu wa Idara ya Ulinzi (DCS) na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa kijeshi, ambapo Rais William Ruto alitangaza siku 3 za maombolezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *