Waziri Mkuu wa Iraq aliyemaliza muda wake, Mohammed Shi’a al Sudani amepinga vikali uhusiano wa aina yoyote ile baina ya nchi yake na utawala pandikizi wa Israeli, akissisitiza kwamba jambo kama hilo halina nafasi katika muundo wa kisiasa wa Iraq wala katika mfumo wa kisheria wa taifa hilo la Kiarabu.

Akizungumza mbele ya jamii ya Wakristo mjini Baghdad kwa mnasaba wa sherehe zao za X-Mass, al Sudani amesisitiza kwamba, msimamo wa Iraq kuhusu masuala ya hatima ya taifa bado ni uleule na haujabadilika na umejikita sana katika maadili na imani za wananchi wa Iraq. Amesisitiza kwamba sera za serikali ya Iraq ni kuliunga mkono taifa la Palestina na Muqawama wake dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Matamshi ya al Sudani yamekuja ili kutoa majibu ya mijadala ya hivi karibuni yaliyozushwa kwa makusudi nchini Iraq ili kuangalia msimamo wa taifa hilo la Kiarabu kuhusu uhusiano wake na utawala dhalimu wa Israel. Israel inaamini kuwa Iraq ni moja ya ardhi zinazopaswa kutekwa na kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni hasa kutokana na kuweko taarifa kwamba, Talmud ambayo ni maandishi makuu ya kidini ya Mayahudi, yaliandikwa katika eneo la Babeli ya Kale ambalo hivi sasa eneo hilo liko kwenye jimbo la Babil la Iraq ya leo.

Iraq haitambui uwepo wa nchi iitwayo Israel, na muda wote Baghdad imekuwa ikipinga vikali majaribio ya kuweko uhusiano wowote rasmi na utawala wa Kizayuni. Huo ni msimamo thabiti wa Wairaq wote ambao wana historia ndefu ya kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina.

Mwaka wa 2022, bunge la Iraq lilipitisha sheria inayoharamisha aina yoyote ya mawasiliano au ushirikiano na taasisi au watu binafsi wa Israel. Hatua hiyo ya Bunge la Iraq iliimarisha msimamo wa muda mrefu wa Baghdad. Tangu wakati huo sheria hiyo imekuwa ikitekelezwa kivitendo na mahakama za Iraq.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *