
Manchester, England. Majeraha ya nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes, ni pigo kubwa kwa timu hiyo kwani itamkosa katika mechi tano, huku kocha wa kikosi hicho, Ruben Amorim akisema: “Ni ngumu kuziba pengo la Bruno Fernandes ambaye tutacheza muda mrefu bila yeye.”
Fernandes alilazimika kutoka katika kichapo cha 2-1, Jumapili iliyopita dhidi ya Aston Villa kutokana na tatizo la msuli wa paja, ambalo Amorim alisema wakati huo litamzuia kiungo huyo wa kati wa Ureno kutokuwepo katika mechi ya leo Ijumaa dhidi ya Newcastle United katika mwendelezo wa Ligi Kuu England.
Licha ya Amorim kukataa kuweka muda mahususi wa kutokuwepo kwa Fernandes alipozungumza na vyombo vya habari juzi Jumatano, ingawa alisema matarajio ni haitachukua muda mwingi kuwa nje, lakini vyanzo mbalimbali vimefichua mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, atarejea uwanjani katika mechi ya Manchester Derby dhidi ya Man City huko Old Trafford, Januari 17, 2026.
“Haitakuwa rahisi kuziba nafasi ya Bruno,” alisema Amorim.
“Niliwaambia hilo asubuhi hii. Tunahitaji kulichukulia jambo hili kwa uzito, kama changamoto ipo watu wanapaswa kusimama na kuwajibika zaidi.”
Katika kipindi cha kuuguza majeraha hayo, Man United itacheza mechi tano bila ya uwepo wa Fernandes ambazo nne ni za Premier dhidi ya Newcastle (Desemba 26, 2025), Wolves (Desemba 30, 2025), Leeds United (Januari 4, 2026), Burnley (Januari 7, 2026) na Brighton (Januari 11, 2026) ikiwa ya Kombe la FA.
Fernandes amekuwa na rekodi ya kipekee ya utimamu wa mwili tangu alipojiunga na klabu hiyo kutoka Sporting Lisbon, Januari 2020.
Katika kipindi cha miaka sita iliyopita, amekosa mechi mbili tu kutokana na majeraha na moja kutokana na ugonjwa, maana yake kutokuwepo kwake kwa sasa kutakuwa ndio muda mkubwa zaidi tangu ajiunge na klabu hiyo ya Old Trafford.
“Si suala la ubunifu tu,” alisema Amorim.
“Katika kila mpira wa adhabu au kona, yeye ndiye anayepanga timu.
“Anaelewa kila nafasi uwanjani, anazingatia kila kitu. Kunapokuwa na mabadiliko, yeye ndiye huwaambia wachezaji wengine wanapaswa kusimama wapi.”
Hili ni pigo kubwa kwa United wakati huu ambao Bryan Mbeumo na Amad Diallo wakiwa nje ya kikosi hicho wakishiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) zinazoendelea nchini Morocco, huku Kobbie Mainoo anayetajwa kuwa ni mbadala wa Fernandes, anauguza jeraha la mguu.