
Waasi wa AFC/M23 wamejiondoa siku ya Alhamisi, Desemba 25, kutoka mji wa Makobola, ulioko kwenye mpaka kati ya maeneo ya Uvira na Fizi (Kivu Kusini). Eneo hili lilidhibitiwa na waasi kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ambayo yalisababisha kutekwa kwa mji wa Uvira.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na vyanzo vya habari kutoka Gazeti la mtandaoni la ACTUALITE.CD, kujiondoa huku kunakuja siku moja baada ya mapigano makali katika vilima vinavyoelekea Kasekezi, Bangwe, Ngalula, na Makobola.
“Tuliwaona wakielekea Uvira na mizigo yao yapata saa nane mchana. Dakika chache baadaye, tuliona wanajeshi wa FARDC na Wazalendo wakiwasili hapa,” chanzo cha kutoka Makobola kikinukuliwa na Gazeti la mtandaoni la ACTUALITE.CD kimesema.
Kwa upande wao, vikosi vya serikali vinasema vimeuteka tena mji wa Makobola na vijiji vinavyozunguka baada ya mapigano yaliyosababisha kupatikana kwa vifaa kadhaa vya waasi na kukamatwa kwa wapiganaji zaidi ya ishirini.
Baada ya kujiondoa kutoka Makobola, waasi wamejikita katika milima ya Lwanga na kwenye vilima vinavyoelekea Kigongo, kijiji cha mwisho kilichopo kilomita 5 kabla ya jiji la Uvira.
Hata hivyo, jeshi lilifanya mashambulizi ya anga leo Ijumaa asubuhi likilenga boti za waasi katika bandari ya Kalundu katika jiji la Uvira.