s

Muda wa kusoma: Dakika 6

Kwa mwaka 2025, BBC Swahili kupitia mfumo wake wa uchambuzi wa usomaji Telescope ilishuhudia ongezeko kubwa la wasomaji katika habari zilizogusa siasa, uchaguzi, usalama, michezo na ubunifu barani Afrika.

Baadhi ya habari zilivuka wasomaji laki tatu, zikionesha maslahi makubwa ya jamii katika masuala yanayogusa maisha yao ya kila siku.

Hizi hapa ni habari 10 zilizosomwa zaidi kwa mwaka 2025, zikiwa zimepangwa kuanzia iliyovutia wasomaji wengi zaidi.

1. CHADEMA, ACT waikataa Tume ya Oktoba 29, CCM yaunga mkono

Wasomaji: Zaidi ya 475,000

Habari hii ilihusu mvutano wa kisiasa ulioibuka baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume Huru ya Uchunguzi kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025. Tume hiyo ilitangazwa Novemba 18, 2025 na ikaongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande pamoja na wajumbe wengine saba waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini, kwenye diplomasia na vyombo vya ulinzi.

Vyama vya upinzani CHADEMA na ACT-Wazalendo vilipinga uteuzi huo vikidai tume hiyo si huru kwa sababu wajumbe wake wote wana uhusiano wa moja kwa moja au wa zamani na serikali na chama tawala cha CCM. Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, alisema kuwa Rais hana uhalali wa kisiasa, kisheria na kimaadili wa kuunda tume ya kuchunguza matukio ambayo, kwa mtazamo wa upinzani, serikali yake inadaiwa kuyahusika.

Kwa upande mwingine, CCM iliunga mkono uundwaji wa tume hiyo ikisisitiza kuwa ni hatua ya kutafuta ukweli na kurejesha amani nchini. Mvutano huu wa hoja kati ya serikali na upinzani uliifanya habari hii kuwa ndiyo iliyosomwa zaidi kupitia BBC Telescope mwaka 2025.

2. Jinsi polisi walivyotumia nguvu kuvunja maandamano Tanzania

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Wasomaji: Zaidi ya 425,000

Habari hii ilikuwa uchunguzi wa kina uliofanywa na BBC Verify kuhusu matumizi ya nguvu na vikosi vya usalama wakati wa kuvunja maandamano yaliyozuka baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025. Ilionesha kwa ushahidi wa video na picha watu wakikimbia kwa hofu, milio ya risasi ikisikika, na raia wakianguka wakiwa wamejeruhiwa, ikiwemo picha ya mwanamke aliyeanguka chini akiwa anatokwa damu.

Uchunguzi huo ulithibitisha video hizo kwa kutumia picha za setilaiti na kulinganisha maeneo, hasa katika mji wa Arusha na maeneo mengine. Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) ilisema imepokea taarifa zinazoonyesha kuwa mamia ya watu waliuawa au kujeruhiwa, huku wengine wakikamatwa katika kipindi hicho cha uchaguzi.

Baada ya intaneti kuzimwa kwa karibu wiki moja, picha na video zilianza kuenea mtandaoni, zikionyesha maafisa wa usalama wakifyatua risasi na miili ya watu ikiwa imetapakaa mitaani. Ukubwa wa ushahidi na uzito wa mada uliifanya habari hii kuvutia wasomaji wengi sana.

3. Fahamu mchakato mzima wa uchaguzi Tanzania 2025

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Zaidi ya wasomaji 330,000

Habari hii ya elimu ya uraia ilieleza kwa kina mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa Tanzania, kuanzia hatua za awali za uteuzi wa wagombea hadi upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo. Iliweka wazi majukumu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa Tanzania Bara na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa upande wa Zanzibar.

Pia makala hii ilifafanua umuhimu wa kampeni, nafasi ya vyama vya siasa, na haki ya wagombea au vyama kupinga matokeo ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria. Ililenga kujibu maswali mengi yaliyokuwepo miongoni mwa wananchi kuhusu uhalali na utaratibu wa uchaguzi.

Kutokana na mazingira ya uchaguzi wa 2025 yaliyokuwa na sintofahamu nyingi, makala hii ikawa rejea muhimu kwa wananchi na ndiyo sababu ilisomwa sana.

4. Nini kimeibadilisha DRC? Safari ya kufuzu Kombe la Dunia

Zaidi ya wasomaji 330,000

Habari hii ilichambua mabadiliko makubwa ya kisoka yaliyoifanya timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufanikiwa kuiondoa Nigeria na kusonga mbele katika mbio za kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026. Mechi hiyo ilimalizika kwa DRC kushinda kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya 1–1.

Makala ilieleza mchango wa wachezaji muhimu akiwemo nahodha Chancel Mbemba na kipa Timothy Fayulu, pamoja na mabadiliko ya kiufundi na kimbinu yaliyoletwa na benchi la ufundi. Ushindi huo uliwapeleka Wakongo katika mechi ya mwisho ya kufuzu baina ya mabara.

Kwa nchi ambayo kwa miaka mingi imekumbwa na changamoto za kisoka, habari hii iligusa hisia za mashabiki wengi barani Afrika.

5. Uchaguzi Tanzania 2025: Uchaguzi huu wa wanawake?

s

Zaidi ya wasomaji 310,000

Habari hii ilihusu tukio la kihistoria katika siasa za Tanzania ambapo wagombea urais wanawake watatu walijitokeza katika uchaguzi mmoja. Rais Samia Suluhu Hassan aliwania muhula wake wa kwanza kama mgombea, akipambana na wagombea wanawake wawili kutoka vyama vya upinzani.

Makala ilimwangazia pia Mwajuma Noty Mirambo wa UMD na Saum Hussein Rashid wa UDP, ikieleza historia zao za kisiasa, ajenda zao na namna walivyobadilisha mjadala wa siasa nchini. Wachambuzi walieleza kuwa hali hiyo ni ishara ya mabadiliko ya kijamii kuhusu kukubalika kwa uongozi wa wanawake.

Upekee wa uchaguzi huo uliifanya habari hii kuvutia wasomaji wengi ndani na nje ya Tanzania.

6. Ndege za Kitanzania zinazoruka kwa mafuta ya bodaboda

s

Zaidi ya wasomaji 250,000

Habari hii ilisimulia ubunifu wa vijana 13 wa Kitanzania waliotengeneza ndege ndogo katika karakana ya uwanja wa ndege wa Mazimbu, Morogoro. Ndege hizo zina injini moja, zinabeba watu wawili na zinatumia petroli ya kawaida inayopatikana kwa urahisi, kama ile ya bodaboda.

Makala ilieleza uwezo wa ndege hizo kuruka umbali mrefu kwa gharama ndogo, kutua kwenye njia fupi hata kwenye majani, na jinsi zilivyoundwa kwa rasilimali chache lakini maarifa makubwa.

Habari hii iliwapa wasomaji picha ya matumaini, ubunifu na uwezo wa vijana wa Kitanzania. Wengi hawakuwa wakiamini kwamba Tanzania inaweza kutengenezwa Tanzania.

7. Heche na Sifuna: Ni pacha wa siasa za upinzani Afrika Mashariki?

S

Chanzo cha picha, FB

Zaidi ya wasomaji 200,000

Habari hii iliwalinganisha John Heche wa Tanzania na Edwin Sifuna wa Kenya kama viongozi wa upinzani wenye mitindo inayofanana ya siasa za uwajibikaji. Ingawa wanatoka nchi tofauti, wote wamejijengea umaarufu kwa kauli kali, hoja nzito na mvuto kwa vijana.

Makala ilieleza kwa nini wanatajwa kama “pacha wa siasa”, ikichambua misimamo yao, historia zao za kisiasa na namna wanavyoikosoa serikali katika nchi zao.

Ulinganisho huu uliibua mjadala mkubwa mtandaoni.

8. Uchaguzi Tanzania 2025: ‘Kampeni za mwaka huu hazina mvuto’

Zaidi ya wasomaji 189,000

Habari hii ilichambua kwa nini kampeni za uchaguzi wa 2025 zilionekana kukosa ushindani na msisimko ukilinganisha na chaguzi zilizopita. Wachambuzi walisema CCM ilitawala uwanja wa kampeni huku vyama vingi vya upinzani vikionekana dhaifu au kukosa rasilimali.

Kujitoa kwa CHADEMA kulibadilisha kabisa taswira ya uchaguzi, na kuufanya kuwa wa kipekee tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

9. Nchi 10 zenye nguvu kubwa zaidi za kijeshi Afrika 2025

s

Zaidi ya wasomaji 159,000

Habari hii ilitokana na ripoti ya Global Firepower iliyopima uwezo wa kijeshi wa nchi 145 duniani. Vigezo vilihusisha idadi ya wanajeshi, silaha, bajeti ya ulinzi, jiografia na teknolojia.

Barani Afrika, Misri, Algeria na Nigeria ziliongoza, zikifuatiwa na Afrika Kusini, Ethiopia na mataifa mengine. Orodha hii iliwavutia wasomaji wengi kutokana na maslahi ya usalama wa bara.

10. Nchi 7 ‘hatari’ zaidi kwa usalama Afrika – 147,000

Zaidi ya wasomaji 147,000

Habari hii ilitokana na Ripoti ya Amani ya Dunia 2025, iliyoonesha kuendelea kudorora kwa amani Kusini mwa Jangwa la Sahara. Migogoro mingi ilielezwa kuwa imefikia viwango vya juu zaidi tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Nchi kama DRC, Sudan Kusini, Mali, Burkina Faso na Somalia zilitajwa kuwa miongoni mwa zilizo hatarini zaidi, jambo lililozua mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wa usalama wa bara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *