
Ingawa mchakato wa kupiga kura nchini Somalia umeanza Disemba 25, hii inaashiria zaidi ya tarehe tu ya uchaguzi.
Inaashiria hatua ya kihistoria ambayo imewawezesha wananchi kwenda kupiga kura ya moja kwa moja baada ya miongo kadhaa.
Kabla ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1969, Somalia ilikuwa moja ya nchi za Afrika zilizokuwa na demokrasia na mfumo wa kisiasa.
Kati ya mwaka 1960 na 1969, nchi hiyo ilifanya uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi, bunge lilifanya kazi kwa ufanisi, na kulikuwa na makabidhiano ya amani ya uongozi wa kisiasa.
Mjadala uliopo leo kuhusu uchaguzi wa watu kushiriki moja kwa moja, ni muendelezo wa demokrasia ambayo iliachwa bila kukamilika mwanzoni mwa kipindi cha nchi hiyo kuwa jamhuri.
Jimbo la Banadir, ambalo linajumuisha mji mkuu wa Mogadishu, wakazi wake wamepiga kura Disemba 25 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 56.
Uchaguzi huu, sio tu, ushindani wa ndani, lakini pia ni hatua muhimu yenye lengo la kuimarisha mfumo wa demokrasia nchini Somalia.
Hatua hii, dhahiri inaonesha azma ya Somalia katika kuwa na mfumo wa uchaguzi wenye kujikita kwa kura ya mtu mmoja mmoja.
Katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa, zaidi ya wagombea 1,600 kutoka vyama 20 vya kisiasa wameshiriki ili kuwakilisha wananchi katika maeneo 16 ya utawala jimbo la Banadir.
Sehemu kubwa ya wagombea walikuwa ni vijana. Hii inaonesha kwamba mustakabali wa Somalia unaendeshwa na kizazi cha vijana.
Siku ya Uchaguzi, takriban watumishi 5000 wa uchaguzi waliopewa mafunzo walikuwa katika vituo vya kupigia kura, huku vikosi vya usalama vipatavyo 10,000 vikipelekwa kuhakikisha mchakato unafanyika kwa utulivu na amani.
Waliokuwa wakisimamia katika vituo vya kura na wapigaji kura, wote walikuwa vijana wa Kisomali.
Hi inaonesha ari ya vijana wa Kisomali kwa mustakabali wa nchi yao lakini pia inaonesha imani ya Somalia ya baadae inayosimamiwa na kizazi cha vijana.
Jinsi msingi wa mchakato ulivyowekwa
Kwa miaka 56 mfululizo, raia wa Somalia walishindwa kuwachagua wale wanaowawakilisha.
Hii ni kufuatia mapinduzi yaliyofanywa na Siad Barre mwaka 1969, siasa za vyama vingi zilifikia ukomo.
Barre alisitisha kwa muda katiba na kuitawala Somalia kwa miaka mingi kupitia mfumo wa chama kimoja.
Wakati huo, raia hawakuwa na sauti yoyote, na Wasomali hawakuwa wanashiriki mchakato wa kisiasa wa kufanya maamuzi.
Wakati huo, hali hii iliyoendelea mpaka 1991, haikuleta demokrasia.
Kinyume chake, Somalia ilisambaratika kabisa, na taifa hilo likaja kujulikana duniani kama kitovu cha migogoro ya kikabila, ukame na ufukara.
Kila mji ukaingia katika himaya ya koo tofauti, makundi na wapiganaji.
Katika miaka ya 2000, huku jamii ya kimataifa ikianza kushughulikia suala la Somalia, uongozi wa mpito ukaanza kutumika. Miongoni mwa mifumo inayotumika ni uwakilishi kwa misingi ya kikoo unaojulikana kama mfumo wa 4.5, ambao unatumika hadi leo. Mfumo huu ulipendekezwa kama hatua ya muda ili kuwaleta pamoja watu wa Somalia ambao walikuwa wamegawanyika.
Kufikia 2012, kuundwa kwa Serikali kuu ya Somalia na katiba ya muda kulidhihirisha mabadiliko makubwa.
Hata hivyo, vitisho vya usalama, hasa kuwepo kwa kundi la kigaidi la Al Shabaab, kulifanya kutimiza lengo hili iwe vigumu kwa kipindi cha muda mfupi. Uchaguzi ambao raia wanashiriki moja kwa moja, ulipangwa kufanyika 2016 na 2020 lakini ukaahirishwa kutokana na sababu za kiufundi na tofauti za kisiasa.