Tunaweza kusema ni mwendelezo wa drama kati ya Diamond Platnumz na Fantana, mrembo kutokea Ghana ambaye hivi majuzi kamjia juu mwanamuziki huyo akikosoa vikali ndoa yake na Zuchu!
Kauli ya Fantana ilikuja kufuatia shoo ya Diamond huko Lagos, Nigeria ambako aliwauliza mashabiki iwapo wanamfahamu mpenzi wake na wengi wakamtaja mrembo huyo lakini staa huyo akajibu siye.
Ni kama kitendo hicho hakikumpendeza Fantana, ndipo akaenda katika Insta Story yake na kumtaka Diamond kuacha kumzungumzia badala yake aendelee na ndoa yake aliyoitaja kama ya uwongo!.
“Umejikita sana kwangu, acha jina langu lipumzike. Niache peke yangu na pambana na ndoa yenu ya uwongo ambayo mnaionyesha kwenye mitandao ya kijamii,” alieleza na kuongeza.
“Kama una furaha ya kweli kwenye ndoa yako feki, kwa nini unanitajataja jukwaani? Kwa nini jina langu liko kila mara mdomoni mwako? Tafadhali acha kulitaja jina langu,” alisema Fantana.
Ikumbukwe mnamo Mei, Diamond aliibua gumzo baada ya kudai yeye na Zuchu walishafunga ndoa kitambo ila hawakuweka wazi kwa wakati huo, hili ni jambo lililoacha maswali kwa wengi.
Sasa ukaribu na drama kati ya Diamond na Fantana vilianza kuonekana katika msimu wa pili wa reality show ya Netflix, Young, Famous & African (2023), ambapo walionekana kuwa na uhusiano wakati huo.
Hata hivyo, ukaribu wao katika shoo hiyo haukumpendeza mzazi mwenziye Diamond, Zari The Bosslady ambaye ana watoto wawili na mwimbaji huyo ambao ni Princess Tiffah (2015) na Prince Nillan (2016).
Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi, alionekana kuvurugwa haswa na uzuri wa Fantana hadi kufikia hatua ya kuibua madai kuwa Zari alikuwa anataka kuzaa naye mtoto mwingine ambaye atakuwa wa tatu kwao!
“Zari alitaka mtoto mwingine na mimi, alitaka kupata mtu wa kumzalia mtoto,” Diamond alimueleza Fantana katika show hiyo ya mastaa wa Kiafrika inayoandaliwa Johannesburg, Afrika Kusini.
Zari alijibu mapigo akimtaja Fantana kama ‘mwanamke wa barabarani’ aliyemchanganya tu Diamond, huku Fantana akidai Zari amefanya upasuaji wa urembo (plastic surgery) kwa mara tano ili afanana nave!
Ikiwa ni zaidi ya miaka miwili tangu hayo yamejiri, bado Fantana anatajwa katika maisha ya Diamond ambaye anaonekana kusonga mbele na Zuchu. Je, huyu Fantana ni nani hasa?
Fantana (Francine Koffe) alizaliwa Julai 3, 1997, na kukulia huko Atlanta, Georgia nchini Marekani ambako alisomea biashara na mitindo, kisha akarudi Ghana ili kufuata ndoto yake ya muziki na mitindo.
Alianza kuandika nyimbo na kuziimba kupitia mitandao ya kijamii, ndani ya muda mfupi alipata mashabiki waliokuwa wakivutiwa na freestyles zake, kisha akaja kuvuma na wimbo wake, Backstabber (2018).
Baadaye Fantana alijiunga na lebo ya Rufftown Records kwa msaada wa Wendy Shay, mwanamuziki maarufu wa Ghana, ndipo akaachia wimbo wake, So What (2019) uliotayarishwa na Mog Beatz.
Aliendelea kuvuma kwenye mahadhi ya Afrobeats kupitia nyimbo zake kama ‘Girls Hate On Girls’, ‘Rich Gyal Anthem’, ‘Fanta My Baby’ na ‘No Dulling’ ambao video yake imetazamwa YouTube mara 617,000.
Mwaka 2023, Fantana alieleza kuwa muziki wake ni Afro-dancehall, akisema amepata msukumo wa kufanya aina hiyo ya muziki kutoka maeneo ya Caribbean, Jamaica na Bahamas.
Mbali na muziki, anaeleza kuwa masuala ya mitindo ni moja ya vipaji vyake vya kuzaliwa, na mara nyingi ameonekana akivalia mavazi ya kisasa na ya kuvutia kama ilivyokuwa ndani ya Young, Famous & African.
Akiongea na mtandao wa Glamour, alisema kupenda kwake televisheni kulimfanya avutiwe na vipindi kama The Real Housewives of Atlanta lakini show ya Young, Famous & African (YFA) ilimkosha zaidi.
“Nilipokaribia kujiunga na YFA, nilifurahi sana kwa sababu nilitoka kuwa mtazamaji wa msimu wa kwanza hadi kuwa mshiriki wa msimu wa pili,” alieleza.
“Ninahisi shoo hii inawapa watu picha nzuri ya mimi ni nani. Pia ni juu yangu kushirikisha dunia kile ninachotaka ijue kunihusu. Hili ni jukwaa zuri sana, hasa kwa vijana wa Kiafrika,” alieleza Fantana.
Mama yake Fantana, Dorcas Affo-Toffey ni mwanasiasa, mjasiriamali, mfadhili (philanthropist), na akijikita katika shughuli za kijamii na uwekezaji kama kununua timu ya soka ya Jomoro FC.
Tangu Januari 7, 2021, amekuwa Mbunge wa Jimbo la Jomoro katika Mkoa wa Magharibi nchini Ghana, na alitangazwa tena mshindi katika uchaguzi wa mwaka 2024.
Ni mwanachama wa National Democratic Congress (NDC) ambacho ni chama cha upinzani na kabla ya siasa, alifanya kazi kama mjasiriamali na kuanzisha biashara kadhaa Marekani na Ghana.