Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kwamba vikosi vya Marekani vimefanya mashambulizi kaskazini magharibi wa Nigeria kulilenga kundi linalojiita dola la kiislam IS ikiwa ni majibu ya kile alichokiita kuwa ni mauaji ya wakristo.
Katika mtandao wa kijamii wa Truth Social, Trump ameandika ” “Marekani imeanzisha mashambulizi makali dhidi ya ISIS Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria, ambao wamekuwa wakiwalenga na kuwaua kikatili Wakristo wasio na hatia”.
Idara ya vita ya Marekani imeachia video inayoonyesha kile kilichoonekana kuwa kombora lililorushwa kutoka kwenye meli ya kivita ya Marekani ingawa hakuna taarifa za awali iliyotolewa kuhusu idadi ya waathirika.
Tukio hili la hivi punde linakuja wakati hali ya ukosefu wa usalama ikiongezeka katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ambayo imekuwa ikikabiliwa na ghasia kwa miaka kadhaa. Itakumbukwa kwamba kundi la kigaidi la Kiislamu laBoko Haram lina mizizi yake nchini Nigeria pia.
Ni tukio lililopangwa muda mrefu
Mapema mwezi Novemba Trump alionya kwamba Washingtoninaweza kuhusika katika mashambulizi hayo, akitoa wito kwa serikali ya Nigeria kuzuia umwagaji damu zaidi na kutishia kwamba isipofanya hivyo itakabiliwa na kupunguzwa kwa misaada.
Hata hivyo, ghasia zimeendelea, huku takriban watu watano wakiuawa na 35 kujeruhiwa katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, msemaji wa polisi katika eneo hilo alisema siku ya Alhamisi.
Kufuatia shambulio hilo la Marekani katika Siku ya Krismasi, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth amesema “anashukuru kwa msaada na ushirikiano wa serikali ya Nigeria.” Kwa mujibu wa Kamandi ya Marekani ya Afrika, walengwa walikuwa katika jimbo la Sokoto la Nigeria.
Kwa upande mwingine, Wizara ya mambo ya nje yaNigeriaimethibitisha mashambulizi hayo ya Markeani dhidi ya kundi linalojiita dola la kiislam.
“Mamlaka za Nigeria bado zinaendelea kushirikiana katika ushirikiano wa kiusalama na washirika wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Marekani, katika kukabiliana na tishio linaloendelea la ugaidi na itikadi kali,” Wizara ya Mambo ya Nje imesema katika taarifa iliyotolewa mapema ijumaa.
Hata hivyo, serikali ya Nigeria na wachambuzi wamekuwa wakikataa kuyataja mauaji ya watu nchini Nigeria kuwa yanasababishwa na itikadi za kidini.