ARUSHA: SHIRIKA Lisilo la Kiserikali la Pingo’s Forum linapanga kutumia zaidi ya Sh milioni 150 kwa ajili ya miradi ya maendeleo pembezoni mwa Wilaya ya Longido mkoani Arusha ikiwemo mradi wa maji na ujenzi wa nyumba za walimu katika wilaya hiyo.
Hayo yalisemwa na Kiaro Tendeu ambaye ni Mratibu wa Pingo’s Forum katika kuimarisha huduma za jamii pembezoni mwa Longido mbele ya Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido na kusema kuwa miradi ya maji iko katika kijiji cha Kimwati kata ya Sinonik na ujenzi wa nyumba na maji katika kata ya Olbomba.

Tendeu alisema katika kata ya Sinonik hadi sasa wameshatumia zaidi ya Sh milioni 70 ujenzi wa chanzo cha maji,ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 na ujenzi wa eneo la kuhifadhi maji kwa ajili ya kunywa mifugo miradi iliyokamilika kwa asilimia 98 kwani Dk Kiruswa anatarajia kuifungua rasmi desemba 31 mwaka huu.
Alisema katika Kata ya Olbomba mbali ya mradi wa maji pia wana ujenzi nyumba za walimu vyote vina gharama ya zaidi ya Sh milioni 80 na miradi yote inatarajiwa kukamilika mwaka huu ili mwakani waendelee na miradi mingine katika kata nyingine zenye changamoto ya maji, elimu na afya.

Dk Kiruswa aliisifu Pingo’s kwa moyo wa kujitoa kwa ajili ya wananchi wa Longido na kuwataka kuendelea na moyo huo kwa vijiji na kata zingine wilayani Longido zenye changamoto mbalimbali kwani serikali itakuwa mstari wa mbele kutoa msaada kwa kile kitakachohitajika pindi wakikwama katika shughuli zao za kila siku.
Alisema Pingo’s Forum ni shirika linalopaswa kuigwa na mashirika mengine yanayaofanya kazi katika wilaya ya Longido katika kuwaletea maendeleo kwani Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yajikite katika shughuli zilizokusudiwa kwa jamii na sio vinginevyo ili jamii iendelee kuwaamini na kuwakubali.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Longido, Thomas Ngobei alisema kuwa ana mpango wa kukutana na NGO’s zote zinazofanya kazi katika wilaya hiyo ili kuwakumbusha malengo na makusudio waliyoyakusudia pindi walipoomba kufanya kazi Longido kwa ajili ya jamii ya wananchi wa wilaya hiyo.