RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa hakuna neema kubwa zaidi ya amani.
Amewahimiza waumini pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kuilinda na kuidumisha neema hiyo kwa maslahi ya Taifa.

Dk Mwinyi ameyasema hayo leo, Desemba 26, 2025, aliposhiriki Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ijumaa Kiembesamaki wa Abdalla Rashid, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameeleza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya Taifa, na kusisitiza kuwa bila amani, jitihada zote za maendeleo haziwezi kufikiwa.

Aidha, amewahimiza waumini na wananchi kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijalia nchi neema ya amani, kama inavyoelekezwa katika Qurani Tukufu.
Katika nasaha zake, amewakumbusha waumini wa Dini ya Kiislamu kuongeza ibada, kumcha Mwenyezi Mungu, na kuimarisha mwenendo mwema katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Rajabu, ambacho ni miongoni mwa miezi mitukufu katika Uislamu.

Dk Mwinyi ameendelea na utaratibu wake wa kujumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Ibada ya Sala ya Ijumaa kwa kusali katika misikiti mbalimbali, kama sehemu ya kuimarisha mshikamano, umoja na maadili ya kidini katika jamii.