
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV amesema katika mahubiri ya Krismasi aliyotoa jana Alkhamisi kwamba anasikitishwa na madhila yanayowafika Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.
Papa Leo amesema, simulizi ya Yesu kuzaliwa katika zizi kunaonesha Mungu “alikita hema lake” miongoni mwa watu wa dunia na kwa mantiki hiyo akahoji: “Inakuaje, sasa, hatuwezi kuangazia mahema ya Gaza, ambayo yanapitia matatizo ya mvua kwa wiki kadhaa, upepo na baridi?”
Kiongozi huyo mpya wa Kanisa Katoliki, ambaye amesherehekea Krismasi yake ya kwanza tangu alipochaguliwa mwezi Mei na makadinali wa dunia kumrithi Papa Francis, katika kipindi cha karibuni amesikika mara kadhaa akieleza kusikitishwa na hali ya Wapalestina huko Ghaza mara na kuwaambia waandishi wa habari mwezi uliopita kuwa suluhisho pekee ya mzozo wa miongo kadhaa kati ya Israel na watu wa Palestina ni kuhakikisha lazima kunakuwepo na taifa la Palestina.
Katika ibada hiyo ya jana Alkhamisi ambapo maelfu ya waumini walikusanyika kwenye Kanisa la St. Peter’s Basilica, Papa Leo alizungumzia pia hali ya watu wasio na makazi kote duniani na uharibifu unaosababishwa na vita katika maeneo mbalimbali duniani…/
“Hali tete ndiyo iko kwa watu wanaoshindwa kujitetea, wamepitia vita vingi, vinavyoendelea na vya zamani, kusababisha kuwepo kwa vifusi na makovu,” alisema papa.