
Polisi wa Zambia apongezwa kwa kukataa hongo ya $50,000 kwenye uwanja wa ndege wa Lusaka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134740-polisi_wa_zambia_apongezwa_kwa_kukataa_hongo_ya_50_000_kwenye_uwanja_wa_ndege_wa_lusaka
Tume ya Kupambana na Rushwa ya Zambia (ACC) imempongeza askari polisi wa kike aliyekataa kupokea hongo ya dola za Kimaarekani 50,000 kutoka kwa mshukiwa wa utakatishaji pesa katika uwanja wa ndege mji mkuu wa nchi hiyo, Lusaka.
2025-12-26T06:14:09+00:00 (last modified 2025-12-26T06:14:09+00:00 )
Dec 26, 2025 06:14 UTC
Tume ya Kupambana na Rushwa ya Zambia (ACC) imempongeza askari polisi wa kike aliyekataa kupokea hongo ya dola za Kimaarekani 50,000 kutoka kwa mshukiwa wa utakatishaji pesa katika uwanja wa ndege mji mkuu wa nchi hiyo, Lusaka.
Sajini Ruth Nyambe, ambaye yuko kwenye Kitengo cha Viwanja vya Ndege, alikataa pesa hizo kutoka kwa mshukiwa, wakati wa taratibu za kiusalama, na inadaiwa mshukiwa huyo alipatikana akiwa na dola milioni $2.3 taslimu na vipande saba vinavyoaminika kuwa vya dhahabu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda.
Polisi nchini Zambia wanasema tukio hilo lilitokea tarehe 5 Februari mwaka huu.
ACC imesema, mshukiwa huyo ambaye jina lake halikutajwa alitaka kumhonga Nyambe dola $5,000 kwanza, lakini alipokataa, mshukiwa huyo akapandisha dau hadi dola $50,000 ili aruhusiwe aendelee na safari yake na fedha hizo.
Kwa mara nyingine tena, Nyambe akakataa, na badala yake akawafahamisha maafisa wa Tume ya Kupambana na Madawa ya Kulevya ya Zambia (DEC), na mshukiwa akakamatwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Lusaka Times, mshukiwa huyo alikuwa anasafiri kutoka Lusaka kuelekea sehemu ambayo haikufahamika.
ACC imempongeza Nyambe na kusema kuwa ni polisi “mwenye weledi wa juu” katika majukumu yake.
Kutokana na uaminifu huo wa maadili ya kazi, Mkurugenzi Mkuu wa ACC Daphne Chabu amemtunukia pia Sajini Nyambe tuzo ya Uadilifu. Haijafahamika kama amepatiwa pia bakhshishi ya pesa au la.
Siku ya Jumatano, Inspekta Jenerali wa Polisi wa Zambia Graphel Musamba alimpandisha cheo Nyambe kutoka Sajini hadi Mkaguzi wa Polisi.
Polisi imesema kupandishwa cheo kwa Bi Nyambe kunaendana na “kutambua uadilifu wake, utendaji kazi, na kukataa kupokea rushwa”…/