HAKUNA kingine kinachohitajika kwa Taifa Stars leo ila ni ushindi tu. Kila Mtanzania bila kujali imani yake, anapaswa kuomba dua njema ili Stars itoboe mbele ya Uganda The Cranes.
Stars inatarajiwa kushuka uwanjani usiku wa leo Jumamosi kucheza mechi ya pili ya Kundi C ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 dhidi ya Uganda huku kila moja ikitoka kupoteza mechi iliyopita mbele ya Nigeria na Tunisia.
Kila moja inahitaji ushindi, lakini kwa Tanzania ni muhimu zaidi ili kuandisha historia mpya katika michuano hiyo, kiasi hata wachezaji wa timu hiyo nao wanakiri wanahitaji dua za Watanzania.
“Kilichobaki kwa sasa tuombeane katika mechi ijayo tulisogeze taifa pale tunapotaka kulisogeza. Naamini tunaweza kuvuka hatua ya makundi.”
Hiyo ilikuwa kauli ya kipa wa timu hiyo, Zuberi Foba akizungumza baada ya kupoteza mechi ya kwanza dhidi ya Nigeria kwa mabao 2-1.
Baada ya kupoteza mechi hiyo ya kwanza, bado haipo mbali na kufikia malengo ya kuingia 16 Bora kwani kutokana na takwimu za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zilipomalizika mechi za raundi ya kwanza, Stars lilikuwa nafasi ya pili kati ya timu nne zinazoweza kupenya kama mshindwa bora.
Ipo hivi. Ukiondoa timu 12 zitakazomaliza nafasi mbili za juu kila kundi ambazo zitafuzu 16 Bora moja kwa moja, kuna nne zitaangaliwa kwa matokeo bora katika kila kundi nazo kufuzu hatua hiyo. Hivyo, kubwa zaidi ni dua za Watanzania ni muhimu Stars kushinda leo kabla ya kuja kumalizana na Tunisia Jumanne ijayo.
Stars na Uganda zitakutana Uwanja wa Al-Barid, Rabat, Morocco kuanzia saa 2:30 usiku kwa saa za Tanzania, mechi hiyo imebeba maana kubwa sana kwa timu zote mbili. Mechi hiyo itatanguliwa na mechi za mapema kati ya Benin na Botswana itakayopigwa saa 9:30 alasiri na ile ya Senegal na DR Congo saa 12:00 jioni zikiwa ni mechi za Kundi D, huku Tunisia na Nigeria zitaumana saa 5:00 usiku.
Baada ya kupoteza mechi ya kwanza kila moja, hii ni nafasi ya kujiuliza na kutengeneza njia bora ya kufuzu hatua inayofuata ambayo kwa Stars ikifanikiwa itakuwa mara ya kwanza, huku Uganda ikiwahi kufika hadi fainali mwaka 1978, lakini ikapoteza mbele ya Ghana kwa mabao 2-0.
Pia ilishuhudiwa mwaka 2019, Uganda ikiishia 16 bora AFCON, fainali zilizofanyika Misri na Stars ilishiriki kwa mara ya pili baada ya miaka 39 na kutoambulia pointi.
Ukiweka kando mafanikio ya Uganda kumaliza ya pili 1978 na kucheza 16 bora 2019, pia 1962 ilimaliza ya nne, hivyo kwa Stars ni muhimu kupata ushindi ili kuisaka rekodi nzuri katika fainali hizi.
Kutoka 2019 hadi sasa Stars imeshiriki AFCON mara ya tatu, wakati Uganda ikiwa ni ya pili baada ya kukosekana 2021 na 2023, huku Stars ikiikosa ya 2021 pekee ndani ya kipindi hicho.
Katika msimamo wa Kundi C, Stars ipo nafasi ya tatu, huku Uganda ikishika mkia japo kila moja haina pointi, ila tofauti ya mabao zimeitenganisha, Stars imefungwa mawili wakati Uganda imeruhusu matatu kupitia kipigo cha 3-1 kutoka kwa Watunisia.
Utamu wa mechi hii unatokana na timu hizo kufahamiana vizuri zikitokea Ukanda wa CECAFA na mara kadhaa zinapokutana na mechi ya kuwa ngumu.
Mechi tano za mwisho zilizokutana katika mashindano na zile za kirafiki, zinaonyesha atakayeshinda basi anaondoka uwanjani bila ya kuruhusu bao, hakukuwa na sare baina yao.
Mara ya mwisho, Stars iliichapa Uganda bao 1-0 katika mechi za kujiandaa na CHAN 2024 iliyochezwa Julai 22, 2025, kabla ya hapo Uganda iliipa Stars kipigo kama hicho katika kufuzu AFCON 2023.
Rekodi zinaonyesha hii ni mara ya kwanza kwa Stars na Uganda kukutana katika michuano ya AFCON, pia ni mara ya pili kushuhudia majirani wa Afrika Mashariki kukutana baada ya 2019 Kenya na Stars kupambana nchini Misri na Kenya kushinda 3-2.
MABADILIKO YA KIUFUNDI
Mechi ya kwanza dhidi ya Nigeria, Stars iliwakosa baadhi ya nyota kwa sababu mbalimbali. Feisal Salum alikuwa anatumikia adhabu ya kadi aliyomalizika na anaweza kucheza dhidi ya Uganda.
Seleman Mwalimu na Yakoub Suleiman majeruhi, hali inayomfanya Foba ataendelea kukaa langoni, Hussein Masalanga akisubiri benchi.
Kurejea kwa Feisal, kunaweza kumpa nafasi Gamondi ya kubadilisha kikosi kutoka kile kilichoanza mechi ya kwanza kilichoonekana kuingia kwa kujilinda zaidi kuliko kushambulia.
Kuwaanzisha viungo wawili wa ukabaji, Alphonce Mabula na Novatus Miroshi, kuliinyima Stars nafasi ya kupandisha mashambulizi kutokana na kukosekana kiungo wa juu mbunifu kariba ya Feisal.
Mechi hii inahitaji kushambulia zaidi kuliko kujilinda, kwani zinahitajika pointi za kuiweka timu sehemu nzuri katika msimamo ikizingatiwa kwamba Tunisia na Nigeria zinazokamata nafasi mbili za juu kwa kukusanya pointi tatu kila moja zinakutana baadaye usiku kwa mechi nyingine ya kundi hilo.
Katika mabadiliko ya kiufundi, Feisal anaweza kuanza badala ya Tarryn Allarakhia ambaye dhidi ya Nigeria alichukua winga moja. Wengine waliobaki wanaweza kuendelea kuwepo japo mabadiliko ya wachezaji hasa kipindi cha pili yanapaswa kufanyika mapema kuongeza nguvu eneo la kushambulia pindi timu ikiwa bado na uhitaji wa mabao au kuimarisha ulinzi kulinda mabao yatakayopatikana.
MTIHANI WA STARS
Baada ya Stars kuanza hatua ya makundi angalau kwa kutikisa nyavu licha ya kupoteza mechi, imeonyesha mabadiliko ya kikosi hicho kwani mara mbili zilizopita, 2019 na 2023, haikuwawahi kufunga bao mechi ya kwanza. Awali ilitikisa nyavu mwaka 1980 dhidi ya Nigeria, imerudia 2025 ikipita takribani miaka 45 huku ikionekana kama vile Nigeria tunawamudu katika kutikisa nyavu zao.
Kilichopo sasa ni Stars kuhakikisha inapata ushindi wake wa kwanza katika AFCON kwani mara zote ilizowahi kushiriki 1980, 2019 na 2023, haijawahi kuonja ladha ya pointi tatu katika mechi moja. Hivyo huu ndiyo wakati wa kaimu kocha mkuu, Miguel Gamondi kuushinda mtihani huo.
Jambo lingine ambalo Stars inapaswa kuepuka nalo ni kuishi kwa mazoea hawa ni majirani zetu tunawamudu. Ilitokea hivyo mwaka 2019 ambapo kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Stars kuongoza 2-1 dhidi ya Kenya, lakini dakika tisini zikawa na maumivu. Kenya 3-2 Tanzania.
Uganda ina nahodha wake, Khalid Aucho, kiungo ambaye anawafahamu vizuri sana nyota wa Tanzania kutokana na kucheza nao muda mwingi ngazi ya klabu hadi timu ya taifa.
Hali hiyo inamhitaji kocha Gamondi aliyewahi kukinoa kikosi cha Yanga na kufanya kazi Aucho kabla ya wote kukutana tena Singida Black Stars kwa sasa kuhakikisha anaweka mbinu nzuri za kumzuia asilete madhara.
Steven Mukwala akiongoza safu ya ushambuliaji ya Uganda, anatokea Simba, anakwenda kukutana na mabeki Ibrahim Hamad, Bakari Mwamnyeto au Dickson Job ambao mara kadhaa wanakutana katika Dabi ya Kariakoo ikiwamo ya Ngao ya Jamii ya msimu huu na Yanga kushinda bao 1-0.