
Shambulio la kigaidi limewalenga waumini waliokuwa katika ibada ya Sala leo Ijumaa katika msikiti wa Imam Ali bin Abi Talib (a.S) katika kitongoji cha Wadi al Dhahab katika mkoa wa Homs , Syria na kuuwa watu 5 na kujeruhi wengine 21.
Shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti kuwa, kwa mujibu wa taarifa za awali watu wasiopungua 5 wameuawa na wengine 21 kujeruhiwa katika mlipuko wa kigaidi katika msikiti wa Imam Ali (a.s) huko Homs.
Televisheni ya al Mayadeen ya Lebanon imenukuu duru za ndani ya Syria na kutangaza kuwa mtu aliyetekeleza shambulio hilo alilipua mada za milipuko ndani ya msikiti wa Imam Ali wakati wakati Sala ya Ijumaa ikiendelea.
Duru za Syria zimearifu kuwa tukio hilo ni shambulizi la kigaidi na kwamba vikosi vya usalama tayari vimeanzisha uchunguzi kuhusu hujuma hiyo katika msikiti wa Imam Ali katika mkoa wa Homs.
Wakati huo huo televisheni ya al Jazira imetangaza kuwa utawala ghasibu wa Israel umelishambulia kwa mizinga na risasi eneo la Tal Ahmar nje kidogo ya mkoa wa Quneitra kusini mwa Syria.
Duru za ndani za Syria pia zimearifu kuwa ndege za kivita za Israe zimeonekana zikiruka mara nyingi katika anga yaa Damascus, mji mkuu wa Syria.
Baada ya kupinduliwa madarakani serikali ya Rais Bashar al Assad, jeshi la utawala wa Kizayuni lilitumia fursa ya ukosefu wa serikali kuu na hali ya ndani ya machafuko na kusonga mbele ndani ya Syria. Kwa mara ya kwanza jeshi la Israel limeikalia kwa mabavu miinuko ya Jabal al-Sheikh huko Syria.
Waziri wa Vita wa Israel Israel Katz Jumatano wiki hii alisema kuwa kamwe hawataondoka katika miinuko hiyo huko Syria.