MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imetoa mafunzo maalumu kwa waganga wafawidhi, wafamasia na wakaguzi wa dawa kutoka wilaya nne za Mkoa wa Tanga. Meneja wa TMDA Kanda ya Mashariki. Keddy Manga, amesema lengo la mafunzo hayo ni kudhibiti matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya ili kuzuia uraibu miongoni mwa vijana.

Wilaya zilizohusika ni Tanga Jiji, Muheza, Pangani na Mkinga. Mafunzo hayo ni mkakati wa serikali kuhakikisha dawa hizo kali ambazo ni muhimu kwa wagonjwa wa upasuaji na saratani, haziingii mitaani kinyume cha sheria. Manga alisema kuwa jukumu la msingi la mamlaka hiyo ni kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi ni bora, salama na vina ufanisi, lakini tahadhari kubwa inahitajika kwenye dawa za maumivu makali.

“Kuna dawa zinatumika kwa wagonjwa wenye maumivu makali kama wa saratani au wanaofanyiwa upasuaji. Hata hivyo, dawa hizi zisipotumika kwa usahihi na kwa kufuata miongozo, zinaweza kusababisha uraibu na kugeuka kuwa dawa za kulevya mitaani,” alisema.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Japhet Simeo amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bombo kwa sasa inahudumia zaidi ya wagonjwa 700 walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya. SOMA: TMDA yatahadharisha matumizi holela ya Dawa

Dk Simeo alionya kuwa baadhi ya wataalamu wasio waaminifu wamekuwa wakichepusha dawa hizo na kuzipeleka mitaani, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa na nguvu kazi ya vijana. “Serikali imeweka utaratibu maalumu wa matumizi ya dawa hizi, wataalamu wetu hawana budi kufuata mwongozo wa udhibiti ili dawa za upasuaji na zile za afya ya akili zisichepushwe.

Matumizi bila maelekezo ya daktari ni sumu inayozalisha waraibu mitaani,” alisema. Naye Mfamasia wa Mkoa wa Tanga, Beatha Kimaro alibainisha kuwa mkoa umeanza kuweka mifumo thabiti ya utunzaji wa dawa hizo chini ya watu maalumu ili kuzuia mianya ya uchepushaji.

Amezitaja baadhi ya dawa zinazofuatiliwa kwa ukaribu kuwa ni zile za jamii ya saikotropiki, narkotiki kama vile pethidaini na mofini, pamoja na dayazepamu (valium), ambazo zote zina uwezo mkubwa wa kuleta uraibu kama zitatumika vibaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *