
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limefanya shambulio la anga dhidi ya wapiganaji wa kundi la DAESH (ISIS) au ISIL kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Katika ujumbe alioweka usiku wa kuamkia leo kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump amesema: “usiku wa leo, kwa maelekezo yangu kama Amiri Jeshi Mkuu, Marekani imefanya shambulio lenye nguvu na hatari dhidi ya wahalifu wa Kigaidi wa ISIS Kaskazini Magharibi mwa Nigeria”.
Katika ujumbe wake huo, Trump amedai kwamba, wapiganaji wa ISIL “waliwalenga na kuwaua kikatili” “hasa Wakristo wasio na hatia, katika viwango ambavyo havijaonekana kwa miaka mingi, bali hata Karne!”
Rais huyo wa Marekani ameendelea kueleza katika ujumbe wake: “nimewaonya hapo kabla magaidi hawa kwamba ikiwa hawatasimamisha mauaji ya Wakristo, watayalipia kwa moto, na usiku wa leo, umekuwepo”.
Wakati huohuo, Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani (AFRICOM), inayohusika na shughuli za jeshi hilo barani Afrika, imeeleza katika ujumbe iliyoweka kwenye mtandao wa X kwamba shambulio la angani lilifanywa “kwa ombi la mamlaka za Nigeria” na limewaua “magaidi wengi wa ISIS”.
Katika taarifa yake, AFRICOM imesema shambulio hilo lilitokea katika “jimbo la Soboto,” ikimaanisha Jimbo la Sokoto nchini Nigeria.
Naye Waziri wa Vita wa Marekani Pete Hegseth amesikika kupitia andiko lake kwenye mitandao ya kijamii akisema: “tunashukuru kwa msaada na ushirikiano wa serikali ya Nigeria,” huku akionya pia kuhusu “mengi yajayo”, yatakayojiri bila kutoa ufafanuzi zaidi…/