Angalau watu 99 waliofungwa baada ya uchaguzi wa urais wa 2024 uliokuwa na utata nchini Venezuela wameachiliwa, mamlaka ya nchi hiyo imetangaza leo Ijumaa.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Watu hawa walikamatwa katika muktadha wa mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na kuchaguliwa tena Julai mwaka uliyopita kwa rais Nicolas Maduro kwa muhula wa tatu, katika uchaguzi uliokumbwa na udanganyifu kulingana na wapinzani wake.

“Serikali na mfumo wa mahakama zimeamua kutathmini kila kesi na, kwa mujibu wa sheria, kutoa hatua za tahadhari, ambazo zimesababisha kuachiliwa kwa raia 99,” Wizara ya Huduma za Magereza imesema katika taarifa. Kulingana na serikali ya Venezuela, watu hawa walifungwa “kwa kushiriki kwao katika vitendo vya vurugu na kuchochea chuki kufuatia uchaguzi wa Julai 28, 2024.”

Karibu watu 2,400 walikamatwa baada ya uchaguzi

Miongoni mwa wafungwa walioachiliwa ni Marggie Orozco, daktari mwenye umri wa miaka 65 aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa “uhaini, uchochezi wa chuki, na njama” baada ya kumkosoa rais kwa ujumbe wa sauti, shirika lisilo la kiserikali la Justicia, Encuentro y Perdón limeliambia shirika la habari la AFP.

Kutangazwa kwa ushindi wa Nicolás Maduro kulisababisha maandamano yaliyosababisha kukamatwa kwa takriban watu 2,400, ambao rais mwenyewe aliwaita “magaidi.” Zaidi ya 2,000 wameachiliwa tangu wakati huo, kulingana na takwimu rasmi.

Wimbi la hivi karibuni la kuachiliwa huru lilianza Siku ya Krismasi, kulingana na Kamati ya Uhuru wa Wafungwa wa Kisiasa (CLIPVE), ambayo imeripoti wafungwa 60 kuachiliwa huru. “Tunasherehekea kuachiliwa huru kwa zaidi ya Wavenezuela 60 ambao hawangepaswa kukamatwa kiholela,” Andreína Baduel aliliambia shirika la habari la AFP siku ya Alhamisi. “Lakini hawako huru kabisa; tutaendelea kufanya kazi kwa ajili ya uhuru wao kamili na wa wafungwa wote wa kisiasa,” aliongeza, akibainisha kwamba watu hawa waliachiliwa huru kwa masharti, huku wakiwa na wajibu wa kuripoti mara kwa mara mbele ya mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *