
Hali ya watoto wa Ukanda wa Ghaza ni ushahidi wa wazi wa janga la kibinadamu na mauaji ya kimbari ya kimfumo yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni kwa muda wa miaka miwili mfululizo mbali na majanga ya kimwili, kisaikolojia, kijamii na kiutamaduni ya wakazi wa ukanda huo. Jinai hizo za Israel zinaendelea hadi hivi sasa kwa sura tofauti.
Kwa zaidi ya miaka 20, Ukanda wa Ghaza uko chini ya mashinikizo ya moja kwa moja ya mashambulizi na kuzingirwa na utawala wa Kizayuni. Watoto katika ukanda huo wamekuwa wakishambuliwa kwa makusudi na kwa sura ya kitaasisi na kuathiriwa moja kwa moja kimwili, kisaikolojia na kijamii kwa kiwango kisicho cha kawaida.
Kuanzia Oktoba 15, 2023 hadi mwishoni mwa 2025, zaidi ya watoto 64,000 huko Ghaza wameuawa shahidi au kujeruhiwa, na wengi wao wamepoteza maisha yao kutokana na kushambuliwa nyumba na maskuli.
Shirika la habari la Mehr limesema kwamba, takwimu hiyo inaonesha tu kiwango cha hasara za kimwili cha mgogoro huo; wakati ambapo watoto wa Ghaza wamo kwenye migogoro mikubwa pia ya kukosa huduma za kimsingi kama vile maji safi, lishe na matibabu. Zaidi ya watu milioni 1 na laki 6, wakiwemo zaidi ya watoto milioni 1, hawapati maji salama wala usafi wa mazingira, hali ambayo imepelekea kuongezeka magonjwa ya kuambukiza na vifo vinavyoweza kuzuilika huko Ghaza.
Kuporomoka mfumo wa elimu Ukanda wa Ghaza
Moja ya athari mbaya za moja kwa moja ya vita ni uharibifu wa mfumo wa elimu. Shule huko Ghaza zimeharibiwa kabisa au zimebadilishwa kuwa makazi ya muda kwa watu waliokimbia makazi yao. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 95 ya skuli za Ghaza zimeharibiwa kikamilifu au zinahitaji ukarabatgi wa kimsingi, na zaidi ya watoto 625,000 wamenyimwa fursa ya kupata elimu rasmi hivi sasa. Madhara ya muda mrefu ya jambo hilo yahaonekana waziwazi. Bila ya elimu, watoto hutumbukia katika hatari ya kudumaa kiakili, kijamii na kisaikolojia, na kuendelea muda mrefu hali hiyo kutapelekea kuongezeka umaskini na kuzuka machafuko yasiyoisha katika vizazi vijavyo.
Mgogoro wa chakula na utapiamlo
Kuendelea kuzingirwa kikamilifu Ukanda wa Ghaza, hasa tangu mwezi Oktoba 2023, kunawasababishia wakati wa ukanda huo matatizo mengine mengi ikiwa ni pamoja na kushindwa kufikishiwa misaada ya dharura kama chakula na madawa na waathiriwa wakubwa ni watoto wadogo. Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limeripoti kwamba zaidi ya asilimia 93 ya watoto wa Ghaza wana uhaba mkubwa wa chakula, na makumi ya maelfu ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wanateseka kwa utapiamlo mkali. Utapiamlo katika umri huo una madhara makubwa na ya muda mrefu; ikiwa ni pamoja na matatizo ya ukuaji wa ubongo usioridhisha, kupungua kwa asilimia 20 ya uwezo wa kujifunza, kudhoofika mifumo ya kinga na kuongezeka hatari ya magonjwa sugu katika siku zijazo. Hizo ni baadhi tu ya madhara yake. Jinai zinazofanywa na Israel za kuwaweka watu na njaa kama silaha ya vita ni ukiukaji wa wazi wa sheria ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu na Mikataba ya Geneva, na athari zake zitadumu kwa vizazi vingi vijavyo.
Kusambaratika mfumo wa afya wa Ghaza
Tangu huko nyuma na hata kabla ya mwezi Oktoba 2023 mfumo wa afya wa Ghaza ulikuwa tayari chini ya mashinikizo makubwa kutokana na ukanda huo kuzingirwa kila upande na Wazayuni. Mashambulizi ya kikatili ya moja kwa moja ya Israel tena ya mujda wa miaka miwili mfululizo yamepelekea zaidi ya asilimia 70 ya vituo vya afya kukosa huduma huko Ghaza. Jinai hizo za Wazayuni zimeongeza hatari ya kuenea magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa watoto, ikiwa ni pamoja na maambukizi ya matatizo ya kupumua, homa ya ini na magonjwa ya ngozi. Kuongezeka vifo vya watoto wachanga, kuzaliwa watoto kabla ya wakati wake na ukosefu wa chanjo ni madhara mengine ya kusambaratika kwa mfumo wa afya huko Ghaza. Hali hiyo si tu inatishia usalama wa kizazi cha hivi sasa, lakini pia inawabebesha Wapaledstina mzigo mzito wa magonjwa na ulemavu kwenye mustakabali.
Ukosefu mkubwa wa makazi ya raia
Israel imefanya uharibifu mkubwa wa nyumba za raia huko Ghaza na kuwanyima watoto zaidi ya milioni moja makazi yao. Hivi sasa zaidi ya watoto 500,000 wanaishi katika mahema ya muda ambayo hayana usalama wowote wala vifaa vya kutia joto au hata huduma ndogo kabisa tena wakati huu wa msimu wa mvua na baridi kali.
Matatizo mengine yaliyosababishwa na mashambulizi ya kikatili na kinyama ya miaka miwili ya Israel huko Ghaza ni pamoja na watoto 50,000 kuuawa shahidi na kujeruhiwa na karibu watoto 40,000 kupata majeraha makubwa na ulemavu wa kudumu.
Madhara mengine ni ulemavu wa akili wa watoto wa Ghaza kiasi kwamba ripoti ya UNICEF inaonesha kwamba asilimia 100 ya watoto katika ukanda huo wana matatizo ya afya ya akili yanayosababishwa na vita. Dalili za kawaida za matatizo hayo ni pamoja na wasiwasi sugu, mfadhaiko, ndoto mbaya na matatizo ya kitabia ambayo yanaweza kuendelea kuwatesa watoto hao hadi wanapokuwa watu wazima.
Kwa mtazamo wa sheria za kimataifa, jinai hizo za Israel za kuwashambulia moja kwa moja watoto wadogo, kuwazuilia chakula na kufanya uharibifu wa miundombinu muhimu ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na Mikataba ya Geneva, na ni jinai za wazi za kivita ambazo watendaji wake wakiongozwa na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wanapaswa kuburuzwa mahakamani na kupewa adhabu kali.