Arusha. Mkazi wa Mtaa wa Ulkung’ uliopo Kata ya Terat, jijini Arusha, Cleofasi Oiso (35) amefariki dunia baada ya kudaiwa kujinyonga nyumbani kwake, huku chanzo kikitajwa kuwa mgogoro wa kifamilia uliotokana na kushindwa kulipa mahari ya mkewe, ambaye wameishi naye kwa miaka minane.

Taarifa zinaeleza kuwa Oiso, aliyekuwa fundi wa kuchomelea alikuwa akiishi na mkewe Anderika Kessy (32) na watoto wao wawili.

Inadaiwa kuwa mgogoro kati yao ulizidi baada ya mkewe kumtaka alipe mahari hata kwa awamu, jambo lililodaiwa kumletea shinikizo kubwa kutokana na hali yake ya kiuchumi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema tukio hilo limetokea jana Desemba 26, 2025 na kwamba, mwili wa marehemu umekutwa ndani ya nyumba yao. Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za jirani na viongozi wa mtaa, kabla ya tukio hilo Oiso alilalamikia mgogoro wake kwa jirani yake na baadaye akamshirikisha Balozi wa mtaa huo, ambaye aliahidi kuitisha kikao cha usuluhishi saa 12 jioni siku hiyo. Hata hivyo, Oiso alifariki kabla ya muda wa kikao hicho kufika.

Akizungumza nyumbani hapo leo Jumamosi Desemba 27, 2025, mke wa marehemu, akiyejitambulisha kwa jina la Anderika, amesema wameishi pamoja kwa miaka minane bila kulipiwa mahari.

Amedai kuwa mgogoro wao umetokana na kumkumbusha mumewe umuhimu wa kumlipia mahari, akieleza kuwa suala hilo ni la heshima na maadili ya ndoa.

Ameongeza kuwa mumewe alikuwa akilalamika kuwa anadaiwa nyumbani kwao Rombo na alikuwa akipitia matatizo mengi ya kiuchumi. “Tulikuwa na mzozo mdogo, lakini sikuwahi kufikiria angefikia hatua hii. Tulikuwa tunavumiliana kwa mambo mengi,” amesema.

Anderika amesema siku ya tukio alikuwa kwa jirani akifanya kazi ndogo, ndipo alipopigiwa simu na Balozi kuhusu madai ya yeye kuondoka nyumbani.

Baada ya kurejea nyumbani, amedai alimkuta mumewe amejining’iniza na juhudi za kuomba msaada hazikufanikiwa.

Kwa upande wake, Balozi wa shina namba 3 katika mtaa huo, Joseph Wilbard amesema kabla ya tukio, Oiso alimtafuta akimwomba msaada wa kuzungumza na mkewe ili asiondoke, akieleza kuwa mgogoro wao unatokana na mahari na maandalizi ya ndoa.

Amesema baada ya kuzungumza na pande zote mbili, walikubaliana kufanya kikao cha usuluhishi jana, lakini Oiso akaamua kujinyonga kabla ya kikao hicho.

Wilbard amewataka wanandoa na vijana kwa ujumla kuepuka kufanya uamuzi wa haraka wanapokabiliwa na changamoto za kifamilia, akisisitiza umuhimu wa kushauriana na kutafuta usaidizi wa wazazi, viongozi wa serikali, dini au  taasisi husika zinazoshughulia matatizo ya familia.

Naye mmoja wa majirani, Evod Assenga amesema kabla hajajinyonga jana, alimweleza kuwa anapitia matatizo makubwa ya kifamilia na kiuchumi, akidai hata siku kadhaa hakuwa amepata chakula.

“Nilimshauri awashirikishe wazazi wa pande zote ili suala la mahari litatuliwe kwa makubaliano ya kulipa kidogo kidogo,” amesimulia jirani huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *