
“Kilichobaki tuombeane katika michezo ijayo tulisogeze Taifa pale tunapotaka kulisogeza. Kwa mimi naamini tunaweza kuvuka hatua ya makundi.” Hiyo ilikuwa kauli ya Zuberi Foba ambaye ni kipa namba moja wa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars alipokuwa akizungumza baada ya kupoteza mechi ya kwanza kundi C katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 dhidi ya Nigeria kwa mabao 2-1.
Stars baada ya kupoteza mechi hiyo ya kwanza, bado haipo mbali na kufikia malengo ya kuingia hatua ya 16 bora kwani kutokana na takwimu za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zilipomalizika mechi za raundi ya kwanza hatua ya makundi, chama letu lilikuwa nafasi ya pili kati ya timu nne zinazoweza kupenya kwa mlango wa uani.
Ipo hivi; ukiondoa timu 12 zitakazomaliza nafasi mbili za juu kila kundi ambazo zitafuzu 16 bora moja kwa moja, kuna nne ambazo zitaangaliwa zenye matokeo bora kila kundi, zitaungana nazo hatua hiyo. Kubwa zaidi, dua za Watanzania ni muhimu chama letu lipate ushindi leo.
Mechi ya leo ambayo Stars itacheza dhidi ya Uganda kwenye Uwanja wa Al-Barid uliopo Rabat nchini Morocco kuanzia saa 2:30 usiku kwa saa za Tanzania, umebeba maana kubwa sana kwa timu zote mbili.
Baada ya kupoteza mechi ya kwanza kila moja, hii ni nafasi yao kujiuliza na kutengeneza njia bora ya kufuzu hatua inayofuata ambayo kwa Stars endapo ikifanikiwa itakuwa mara ya kwanza, huku Uganda ikiwahi kufika hadi fainali mwaka 1978, lakini ikapoteza mbele ya Ghana kwa mabao 2-0.
Pia ilishuhudiwa mwaka 2019, Uganda ikiishia hatua ya 16 bora katika AFCON, fainali zilizofanyika nchini Misri ambapo Stars ilishiriki kwa mara ya pili baada ya kupita takribani miaka 39.
Ukiweka kando mafanikio ya Uganda kumaliza nafasi ya pili 1978 na kucheza 16 bora 2019, pia 1962 ilimaliza nafasi ya nne, hivyo kwa Stars ni muhimu kupata ushindi ili kuisaka rekodi nzuri zaidi katika fainali hizi.
Kutoka 2019 hadi sasa, Stars imeshiriki AFCON mara ya tatu, wakati Uganda ikiwa ya pili baada ya kukosekana 2021 na 2023, huku Stars ikiikosa ya 2021 pekee ndani ya kipindi hicho.
Katika msimamo wa kundi C, Stars inakamata nafasi ya tatu, huku Uganda ikiwa ya mwisho zote zikiwa hazina pointi, lakini tofauti ya mabao ndiyo inazitenganisha timu hizo. Stars ilifungwa 2-1, wakati Uganda ikichapwa 3-1 na Tunisia.
Utamu wa mechi hii unakuja kutokana na timu hizo kufahamiana vizuri zikitokea Ukanda wa CECAFA na mara kadhaa zinapokutana, haijawahi kuwa rahisi.
Baada ya mwaka huu mataifa hayo kuandaa kwa pamoja michuano ya CHAN sambamba na Kenya, zinapambana kuhakikisha zinafanya vizuri katika AFCON ya mwaka huu kabla ya 2027 kuandaa tena kwa pamoja.
Mechi tano za mwisho zinaonyesha timu hizo katika kukutana kwenye mashindano na zile za kirafiki, zinaonyesha yule atakayeshinda basi anaondoka uwanjani bila ya kuruhusu bao, hakukuwa na sare baina yao.
Mara ya mwisho, Stars iliichapa Uganda bao 1-0 katika mechi za kujiandaa na CHAN 2024 iliyochezwa Julai 22, 2025, kabla ya hapo, Uganda iliipa Stars kipigo kama hicho katika kufuzu AFCON 2023.
Rekodi zinaonyesha hii ni mara ya kwanza kwa Stars na Uganda kukutana katika fainali za AFCON, huku pia ni mara ya pili kushuhudia majirani wa Afrika Mashariki kukutana baada ya 2019 Kenya na Stars kupambana nchini Misri na Kenya kushinda 3-2.
Mechi ya kwanza dhidi ya Nigeria, Stars iliwakosa baadhi ya nyota wake kwa sababu mbalimbali. Feisal Salum alikuwa anatumikia adhabu ya kadi ambayo imemalizika na anaweza kucheza dhidi ya Uganda.
Seleman Mwalimu na Yakoub Suleiman majeruhi huku Yakoub ambaye ni kipa, inaelezwa majeraha yake makubwa hivyo Foba ataendelea kukaa langoni, Hussein Masalanga akisubiri benchi.
Kurejea kwa Feisal, kunaweza kumpa nafasi Gamondi ya kubadilisha kikosi kutoka kile kilichoanza mechi ya kwanza ambacho kilionekana kuingia kwa kujilinda zaidi kuliko kushambulia.
Kuwaanzisha viungo wawili wa ukabaji, Alphonce Mabula na Novatus Miroshi, iliinyima Stars nafasi ya kupandisha mashambulizi kutokana na kukosekana kiungo wa juu mbunifu kariba ya Feisal.
Mechi hii inahitaji kushambulia zaidi kuliko kujilinda kwani zinahitajika pointi za kuiweka timu sehemu nzuri katika msimamo ikizingatiwa kwamba Tunisia na Nigeria zinazokamata nafasi mbili za juu kwa kukusanya pointi tatu kila moja, zinakutana zenyewe baadaye baada ya kushuhudia matokeo ya majirani hao.
Katika mabadiliko ya kiufundi, Feisal anaweza kuanza badala ya Tarryn Allarakhia ambaye dhidi ya Nigeria alichukua winga moja. Wengine waliobaki wanaweza kuendelea kuwepo japo mabadiliko ya wachezaji hasa kipindi cha pili yanapaswa kufanyika mapema kuongeza nguvu eneo la kushambulia pindi timu ikiwa bado na uhitaji wa mabao, au kuimarisha ulinzi kulinda bao au mabao yatakayopatikana.
Baada ya Stars kuanza hatua ya makundi angalau kwa kutikisa nyavu licha ya kupoteza mechi, imeonyesha mabadiliko ya kikosi hicho kwani mara mbili zilizopita, 2019 na 2023, haikuwawahi kufunga bao mechi ya kwanza. Awali ilitikisa nyavu mwaka 1980 dhidi ya Nigeria, imerudia 2025 ikipita takribani miaka 45 huku ikionekana kama vile Nigeria tunawamudu katika kutikisa nyavu zao.
Kilichopo sasa ni Stars kuhakikisha inapata ushindi wake wa kwanza katika AFCON kwani mara zote ilizowahi kushiriki 1980, 2019 na 2023, haijawahi kuonja ladha ya pointi tatu katika mechi moja. Hivyo huu ndio wakati wa kaimu kocha mkuu, Miguel Gamondi kuushinda mtihani huo.
Jambo lingine ambalo Stars inapaswa kuepuka nalo ni kuishi kwa mazoea kwamba hawa ni majirani zetu tunawamudu. Ilitokea hivyo mwaka 2019 ambapo kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Stars kuongoza 2-1 dhidi ya Kenya, lakini dakika tisini zikawa na maumivu. Kenya 3-2 Tanzania.
Uganda ina nahodha wake, Khalid Aucho, kiungo ambaye anawafahamu vizuri sana nyota wa Tanzania kutokana na kucheza nao muda mwingi ngazi ya klabu hadi timu ya taifa.
Hali hiyo inamuhitaji kocha Gamondi ambaye anamfundisha Aucho pale Singida Black Stars huku pia akimnoa katika kikosi cha Yanga walipokuwa wote pamoja, kuhakikisha anaweka mbinu nzuri za kumzuia asilete madhara.
Steven Mukwala akiongoza safu ya ushambuliaji ya Uganda, anatokea klabu ya Simba, anakwenda kukutana na mabeki Ibrahim Hamad, Bakari Mwamnyeto au Dickson Job ambao mara kadhaa wanakutana katika Dabi ya Kariakoo.