
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali shambulio la kigaidi dhidi ya Waislamu katika Msikiti wa Imam Ali ibn Abi Talib (AS) katika Mkoa wa Homs nchini Syria ambalo limeua shahidi na kujeruhi watu wengi wakati wa Sala ya Ijumaa ya jana Msikitini humo.
Esmaeil Baghaei ametoa taarifa akitangaza msimamo wa kimsingi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kupinga na kulaani aina zote za ugaidi na misimamo mikali na kusema kwamba, wahusika wakuu wa jinai kama hizo ni madola ya kigeni yaliyoivamia Syria na vitendo vyao vya mara kwa mara vya kutoheshimu uhuru wa nchi hiyo ya Kiarabu. Vitendo hivyo vimeandaa mazingira ya kuendelea kuwepo, kukua na kuenea magenge ya kigaidi na yenye misimamo mikali nchini humo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa matamshi hayo akiilenga moja kwa moja Marekani na Israel kwa kuivamia kijeshi Syria na kufanya mashambulio ya mara kwa mara nchini humo.
Amesema, jinai za Israel za kushambulia mara kwa mara miundombinu ya kiraia na kiulinzi ya Syria na kukalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kwa kisingizio cha kuzuia kuenea machafuko ni sababu kuu ya kupata nguvu magenge ya kigaidi nchini Syria.
Marekani pia imeanza kushambulia maeneo mbalimbali ya Syria kwa madai ya kupambana na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) lakini wachambuzi wanasema, lengo hasa la Washington ni kujizatiti kijeshi nchini Syria hasa kwenye visima vya mafuta ili iweze kupora zaidi utajiri wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametaka kusakwa na kuadhibiwa wahusika wote wa shambulio la jana Ijumaa la Msikitini huko Homs Syria wakiwemo wale waliopanga na walioliamuru kufanyika jinai hiyo, akisisitiza kwamba watawala wa hivi sasa wa Syria wana jukumu la kulinda usalama wa raia.
Shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti kwamba, watu wasiopungua watano wameuawa na wengine 18 kujeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi lililotokea Msikitini katika kitongoji cha Wadi al-Dhahab huko Homs, magharibi mwa Syria wakati wa Sala ya Ijumaa ya jana.