Israel imetangaza siku ya Ijumaa, Desemba 26, kuitambua Somaliland, jamhuri iliyojitangaza kujitawala. Hadi sasa, jamhuri hii, ambayo ilijitenga na Somalia karibu miaka 35 iliyopita, haijawahi kutambuliwa kama taifa.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Israel inakuwa taifa pekee duniani linaloitambua Somaliland kama “taifa huru na linalojitawala,” utambuzi ambao ni “wa pande zote mbili,” kulingana na taarifa rasmi ya Israel.

Katika taarifa hii, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anarejelea “moyo wa Makubaliano ya Abraham,” akimaanisha wimbi la kuhalalisha ambalo lilishuhudia Falme za Kiarabu, Bahrain, Morocco, na Sudan zikianzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel mwaka wa 2020. Sudan, ambayo tangu wakati huo imekuwa ikikumbwa na vita, haijaidhinisha kufufua  uhusiano huu.

Kwa upande wa athari, kutambuliwa kwa Somaliland hakuhusiani sana na matarajio ya kufuua uhusiano na Saudi Arabia, ambayo kwa muda mrefu ilitarajiwa na Israeli lakini kwa sasa imezuiwa na Riyadh kutokana na sera ya taifa la Kiyahudi kwa Wapalestina.

Kwa kuimarisha uhusiano na Somaliland, Israel inaweza kutumaini kupata nafasi katika Pembe ya Afrika, karibu na waasi wa Houthi huko Yemen, washirika wa Iran na maadui waliotangazwa wa taifa la Kiyahudi. Pia kuna ripoti ambazo hazijathibitishwa za mpango wa kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza hadi Somaliland, mojawapo ya matukio yaliyosambaa katika miaka ya hivi karibuni huku maafisa wa Israel na Marekani wakijadili waziwazi kuhusu Ukanda wa Gaza kuachwa bila watu wote au sehemu ya wakazi wake.

Shutma kutoka Somalia

Kuanzia na shutma za Somalia yenyewe. Mogadishu inaona utambuzi wa Israel kwa Somaliland kama “shambulio la makusudi” dhidi ya uhuru wake. Kulingana na taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia, utambuzi huu unazidisha “mvutano wa kisiasa na usalama katika Pembe ya Afrika, Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden, Mashariki ya Kati na kikanda katikauelewa pana.” Somalia pia ilibainisha tena uungaji mkono wake kwa raia wa Palestina.

Nje ya Somalia, shutma ziliongezeka jioni ya jana, haswa kutoka Djibouti, Misri, na Uturuki, ambazo zililaani “uingiliaji wa waziwazi” katika masuala ya Somalia. Mawaziri wa mambo ya nje wa Somalia, Misri, Uturuki, na Djibouti walizungumza kwa simu baada ya tangazo la Israel, wakielezea “kufutilia mbali kabisa hatua hiyo  ya Israel na kulaani utambuzi wa Israel wa eneo la Somaliland,” na kusisitiza “uungaji mkono wao kamili kwa umoja, uhuru, na uadilifu wa eneo la Somalia.”

Kulingana na taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre, utambuzi wa Israel kwa Somaliland pia unazidisha “mvutano wa kisiasa na usalama katika Pembe ya Afrika, Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden, Mashariki ya Kati, na kikanda katika uelewa pana.”

Mashirika kadhaa pia yamefutilia mbali utambuzi wa Israel kwa Somaliland, ikiwa ni pamoja na Baraza la Ushirikiano la Ghuba, Jumuiya ya Kiarabu, na Umoja wa Afrika. Katika taarifa, Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahmoud Ali Yousouf wa Djibouti, alithibitisha tena kujitolea kwa AU kwa umoja wa Somalia. Alielezea hatua hiyo kuwa kinyume na kanuni za Umoja wa Afrika, ambayo inahatarisha kuunda “mfano hatari” wenye matokeo makubwa kwa amani na utulivu kote barani.

Somaliland ilitangaza uhuru wake kwa upande mmoja mnamo mwaka 1991, huku Jamhuri ya Somalia ikiingia katika machafuko kufuatia kuanguka kwa utawala wa kijeshi wa Siad Barre. Tangu wakati huo imekuwa ikifanya kazi kwa uhuru, ikiwa na sarafu yake, jeshi na polisi, na inajulikana kwa utulivu wake ikilinganishwa na Somalia, ambayo inakabiliwa na uasi wa Kiislamu wa Al Shabab na migogoro sugu ya kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *