Utawala wa Kizayuni wa Israel umetangaza kutambua eneo la Somalia la ‘Somaliland, ambalo limejitangazia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili.

Hatua hiyo ya utawala haramu wa Israel imekabiliwa na upinzani mkali kutoka Somalia na mataifa kadhaa ya eneo hilo,  ambayo yameonya kuwa inakiuka sheria za kimataifa na kutishia uthabiti wa kieneo.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilisema Ijumaa kwamba Tel Aviv imetambua rasmi Somaliland kama “taifa huru na lenye mamlaka kamili” na kusaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia.

Netanyahu alihusisha uamuzi huo na “Mkataba wa Abraham” ulioanzishwa na Rais wa Marekani Donald Trump katika urais wake wa kwanza, akisema ndio msingi wa kutambua Somaliland.

Somalia siku ya Ijumaa ilipinga vikali kile ilichoeleza kuwa ni hatua isiyo halali ya Israel kutambua eneo lake lililojitenga, Somaliland, kama taifa huru. Serikali ya Mogadishu imetaja uamuzi huo kuwa ni uvunjaji wa mamlaka na umoja wa ardhi ya taifa.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia imesisitiza “msimamo thabiti na usioweza kujadiliwa wa kulinda mamlaka, umoja wa kitaifa na mipaka ya ardhi ya Somalia.” Taarifa hiyo imeashiria Katiba ya Muda ya Somalia, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na Mkataba wa Msingi wa Umoja wa Afrika kama msingi wa kisheria wa msimamo huo.

Upinzani wa kieneo

Umoja wa Afrika (AU) siku ya Ijumaa umepinga vikali jaribio lolote la kutambua eneo lililojitenga la Somaliland kama taifa huru, ukisisitiza tena dhamira yake thabiti ya kulinda umoja, mamlaka na mipaka ya ardhi ya Somalia.

Katika taarifa iliyotolewa, Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahmoud Ali Youssouf, alisisitiza bila shaka msimamo wa umoja huo kuhusu “heshima kwa mipaka isiyoguswa iliyoachwa baada ya uhuru.”

Taarifa hiyo ilisema Youssouf “anakataa kwa dhati mpango au hatua yoyote ya kutambua Somaliland kama chombo huru, akisisitiza kuwa Somaliland bado ni sehemu kamili ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia.”

Iliongeza: “Jaribio lolote la kudhoofisha umoja, mamlaka na mipaka ya ardhi ya Somalia linapingana na misingi ya msingi ya Umoja wa Afrika na lina hatari ya kuanzisha mfano hatari wenye athari kubwa kwa amani na uthabiti barani Afrika.”

Wakati huo huo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (P-GCC) pia zililaani hatua ya Israel, zikisema ni “ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na uvunjaji wa wazi wa kanuni za umoja na mamlaka ya mataifa.”

Katibu Mkuu wa Arab League, Ahmed Aboul Gheit, alieleza kuwa kutambua Somaliland ni “kosa kubwa linalodhoofisha misingi ya sheria za kimataifa.” Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi nalo  limeonya kuwa hatua hiyo ni “hatari kwa uthabiti wa Somalia na eneo lote la Pembe ya Afrika.”

Muktadha wa kihistoria na kijeshi

Somaliland, iliyojitenga na Somalia tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1991, imekuwa ikijitawala lakini haijapata kutambuliwa kimataifa. Iko kando ya Ghuba ya Aden na inamiliki bandari ya kimkakati ya Berbera.

Ripoti zinaeleza kuwa Israel inapanga kujenga kituo cha kijeshi katika Somaliland, hatua ambayo itaiwezesha kudhibiti eneo muhimu la kistratijia la Ghuba ya Aden na kuendesha mashambulizi dhidi ya serikali ya Ansarullah nchini Yemen. Aidha utawala wa Israel unalenga kutekeleza mpango wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka Gaza hadi Somaliland ikiwa ni katika fremu ya sera zake za maangamizi ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *