
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kutumia zaidi ya Sh50 bilioni kujenga Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, bado mabasi hayo yanaendelea kushusha na kupakia abiria nje ya kituo na hivyo kukikosesha mapato.
Kufuatia hali hiyo, Serikali imeunda timu maalumu ya wataalamu itakayofanya tathmini ya kina ya uendeshaji wa stendi hiyo, itakayofanya kazi kwa siku 90.
Kituo hicho, kilichoanza rasmi kutoa huduma Februari 24, 2021, kilijengwa kwa lengo la kuboresha usafiri wa mabasi ya mikoani, kuondoa msongamano barabarani na kuweka utaratibu wa kisasa wa usafiri wa umma mikoani.
Hata hivyo, zaidi ya miaka minne tangu kifunguliwe, changamoto ya mabasi kutokitumia kituo hicho kushusha na kupakia abiria imeendelea kuwa mfupa uliokosa meno ya kuutafuna.
Ukiacha kukosa mapato yanayoenda kwenye Manispaa ya Ubungo, wajasiriamali na wakazi wa eneo hilo, wanasema hatua ya mabasi kupakia abiria nje ya kituo hicho, inaathiri biashara zao na malengo ya mradi.
Ni mfupa mgumu
Mei 30, mwaka 2022, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa, alitoa siku saba kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kukutana na wadau kuweka utaratibu wa mabasi kushusha na kupakia abiria ndani ya kituo.
Katika maelekezo hayo, alitaka mkuu huyo wa mkoa akutane na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) na wadau wengine.
Katika ziara yake kituoni hapo, Bashungwa alisisitiza Serikali haitakubaliana na watu wasiofuata utaratibu uliowekwa, ikizingatiwa fedha nyingi zilitumika kujenga stendi hiyo.
Aidha, aliagiza kufanyiwa mapitio kiwango cha kodi ya pango kwa wapangaji wa stendi hiyo, kuondolewa kwa magari mabovu zaidi ya 40 yaliyokuwa yameegeshwa kwa muda mrefu na kuimarishwa kwa usimamizi wa shughuli za stendi hiyo.
Hivyo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla alitangaza kuondoa katazo lililokuwa likizuia mabasi kupakia abiria au kushusha katika vituo binafsi na badala yake aliruhusu utaratibu huo kuendelea kwa sharti la kila basi kuingia ndani ya kituo cha Magufuli.
Uamuzi huo ulitolewa Agosti mwaka 2022 wakati wa kikao cha pamoja baina ya Latra, wamiliki wa stendi binafsi na Manispaa ya Ubungo na kubaini pasipokuwa na shaka kuwa, waliotengeneza vituo binafsi walifuata taratibu na kupatiwa vibali baada ya kukidhi vigezo.
Miongoni mwa vigezo vilivyotolewa na Latra ili kuruhusiwa kuanzisha stendi binafsi ni kuwepo kwa vyoo, sehemu ya mapumziko kwa abiria, viburudisho na sehemu ya maegesho.
Kutokana na hilo, Makalla aliridhia vituo binafsi vitano vilivyohakikiwa kuendelea kutoa huduma na kufungua milango kwa wamiliki wengine wanaohitaji kuwa na vituo binafsi kushirikiana na Latra waanzishe.
Aidha, Makalla aliiagiza Manispaa ya Ubungo kukaa kikao mara moja na wamiliki wa stendi binafsi ili kuona njia bora ya ukusanyaji wa mapato.
Baada ya yote hayo, mwenendo wa mabasi kushusha na kupakia abiria nje ya stendi umeendelea kuwepo.
Malalamiko mapya
Mjasiriamali katika kituo hicho, John Joseph, amesema mabasi mengi bado yanaegeshwa nje ya stendi badala ya kuingia ndani kama ilivyoelekezwa.
“Ni muda mrefu tangu tulipohamia hapa, lakini changamoto hii bado ipo. Mabasi mengi yanabaki nje badala ya kuingia stendi. Tunaomba Serikali itusaidie kulisimamia hili,” amesema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mshikamano, Herny Madenge amesema stendi hiyo ingeleta tija zaidi endapo mabasi yote yangelazimishwa kuitumia kikamilifu.
“Natamani sana mabasi yote yaishie hapa. Stendi ipo, miundombinu ipo, lakini matumizi yake bado ni hafifu,” amesema.
Wamiliki wa mabasi wanena
Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo amesema kumekuwa na ongezeko la mabasi yanayoihama stendi ya Magufuli na kuegesha pembezoni mwa hifadhi za barabara, kinyume cha utaratibu.
Ametaja maeneo ya Shekilango na Manzese kuwa miongoni mwa yanayotumiwa na baadhi ya mabasi kushusha na kupakia abiria bila kuingia stendi.
“Kuna mabasi yanayoanza safari na kupita Bagamoyo moja kwa moja bila kufika hapa stendi. Kwanza yanakwepa ushuru, pia kuna vibali vingi vinazidi kutolewa vya mabasi kuegeshwa nje ya stendi,” amesema Mwalongo.
Amesema stendi hiyo ilijengwa kwa gharama kubwa, hivyo ni muhimu mabasi yote ambayo hayajakidhi vigezo vya kuwa na vituo binafsi yaingie ndani ya kituo hicho.
“Hili si suala la Taboa pekee, nimezungumza kama mdau wa stendi. Kama hali itaendelea hivi, stendi ya Magufuli itakufa kwa sababu hakuna gari litakaloingia hapa,” amesema.
Hata hivyo, amesema yapo mabasi machache ambayo yamekidhi vigezo vya kuwa na vituo vyake binafsi, ikiwamo sehemu za kupumzika na huduma za chakula, lakini akadokeza mengi hayana sifa hizo.
“Wengine mtu ana ofisi moja tu, lakini anaegesha mabasi yake nje ya stendi. Hii si sawa,” amesema.
Uchunguzi kufanyika
Kutokana na malalamiko hayo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Reuben Kwagilwa, amemwagiza Katibu Mkuu, Adolf Ndunguru, kuunda timu maalumu ya wataalamu itakayofanya tathmini ya kina ya uendeshaji wa stendi hiyo.
Katika ziara yake kituoni hapo Desemba 23, 2025, Kwagilwa alisema timu hiyo itashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na itajumuisha wataalamu wa sekta ya usafiri, watumiaji wa stendi na taasisi nyingine za Serikali zenye dhamana ya usafiri wa umma.
“Ifanyike tathmini ya mradi huu, ikihusisha malengo yake ya awali, ufanisi wake, miundombinu iliyopo, huduma zinazotolewa na mapato yanayopatikana na yanayopotea,” amesema.
Alisema timu hiyo itapewa siku 90 kufanya kazi yake na kutoa mapendekezo yatakayosaidia Serikali kupata suluhisho la kudumu kuhusu matumizi sahihi ya stendi hiyo.
“Changamoto zote mlizozitoa nimezipokea kwa niaba ya Waziri. Tuipe nafasi timu hii ifanye kazi ili tupate mwelekeo sahihi wa kwenda mbele kutoka hapa tulipo,” alisema.