
Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Shiraz katika Mkoa wa Fars, Iran, kimechukua hatua kubwa za kubadilisha jiji hili kuwa kitovu cha utalii wa matibabu katika Asia Magharibi kwa kufikia makubaliano ya ushirikiano na Uzbekistan na kupanga kupanua mazungumzo na nchi zingine jirani.
Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Shiraz katika Mkoa wa Fars, kusini mwa Iran, kimeharakisha njia ya kuibadilisha Shiraz kuwa moja ya vitovu vikuu vya utalii wa kimatibabu Asia Magharibi, ndani ya mfumo wa mpango wa muda mrefu na kutegemea uwezo wake wa kisayansi na kimatibabu. Kulingana na Pars Today, njia hii ya kimkakati imeundwa kwa lengo la kuvutia wagonjwa wa kimataifa na kukuza ushirikiano wa mpakani katika uwanja wa afya.
Abdul Khaleq Keshavarzi, Mkurugenzi wa Usimamizi na Maendeleo ya Rasilimali katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Shiraz, ametangaza katika mahojiano na IRNA kwamba, chuo kikuu hicho kimesaini mkataba wa makubaliano na Uzbekistan na kinafanya kazi ya kupanua ushirikiano wa kisayansi na kimatibabu na nchi jirani. Alisema: “Chuo kikuu hiki kimeazimia kuvutia wagonjwa zaidi Shiraz kwa matibabu kwa kuanzisha ofisi za pamoja na kuwezesha kupelekwa kwa maprofesa zaidi chuoni hapo.”
Keshavarzi aliongeza: Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Shiraz kinajaribu kuingia katika mazungumzo na Uzbekistan, Tajikistan, Oman, Qatar na nchi za kikanda katika uwanja wa utalii wa kimatibabu, na ofisi za pamoja zitaanzishwa na nchi hizi; sasa imeidhinishwa na Kamati ya Utalii kwamba maprofesa wa chuo kikuu wanaweza kwenda katika nchi hizi kuwatembelea wagonjwa.
Mkurugenzi wa usimamizi na maendeleo ya rasilimali katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Shiraz aidha amesema: Bila shaka, tumeazimia kuwatibu wagonjwa nchini Iran, si madaktari wetu kwenda katika nchi hizo na kufanya taratibu za upasuaji au matibabu.