MWANAMKE aliyefahamika kwa jina la Joyce Mwasumbi, mkazi wa Kijiji cha Kanazi wilayani Nkasi mkoani Rukwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kitenge chumbani kwake.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kanazi, Rudis Ulaya amesema tukio la mwanamke huyo ambaye ni mke wa Mchungaji wa Kanisa la EAGT, Ibrahimu Mwaipopo katika kijiji hicho kujinyonga limetokea Desemba 24, mwaka huu saa 2:00 asubuhi, baada ya mumewe kwenda kanisani kupalilia pembeni mwa jengo la kanisa hilo.
Alisema wakati mumewe akiendelea na jukumu lake kanisani, mkewe aliutumia mwanya huo kujitundika kwa kutumia kitenge na muda mfupi, mumewe aliingia chumbani huko na kumkuta akiwa amejitundika juu huku akitapatapa kufa, ndipo alipochukua kisu na kukikata kitenge hicho kwa lengo la kuokoa uhai wake lakini muda mfupi alipoteza maisha.
Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa baada ya yeye kumhoji mume wa marehemu, Mwaipopo alidai kuwa huenda kifo chake kimetokana na deni alilokuwa nalo.
Alisema alikopa fedha za kanisa hilo na siku za hivi karibuni, alionesha kukosa furaha kutokana na deni hilo na kuwa huenda jambo hilo likasababisha mwanamke huyo kujinyonga.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Shadrack Masija amethibitisha tukio hilo na kusema jeshi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi kilichosababisha mwanamke huyo kujinyonga.
Pia, ameishauri jamii kushirikisha watu pale wanapokumbwa na changamoto mbalimbali, badala ya kuchukua maamuzi magumu kama hayo ya kujitoa uhai.
