Chama cha Waandishi wa Habari cha Palestina kimeulaani utawala wa Israel kwa kufuata sera ya kimfumo ya kuwalenga waandishi wa habari, kikisema ukatili unaofanywa dhidi ya vyombo vya habari umeongezeka sana mwaka 2025 kama sehemu ya njama za kuzuia ripoti za Wapalestina.

Katika taarifa iliyotolewa jana Ijumaa, Kamati ya Uhuru ya chama hicho ilisema askari wa Israel wamevuka kipindi cha kuzuia kazi za wandishi wa habari na sasa wanatekeleza sera ya “kuwanyamazisha waandishi wa habari kupitia mauaji, kuwajerahi, na kuwatia ulemavu wa kudumu.”

Kamati hiyo imesema, lengo ni kuzuia harakati yoyote ya kuandika na kusajili matukio yanayojiri na kudhoofisha simulizi ya Palestina.

Kwa mujibu wa tarifa ya shirika hilo, kufikia mwisho wa Novemba 2025, waandishi habari wasiopungua 76 wa Kipalestina walikuwa wameuawa au kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel.

Kamati hiyo imezitaja takwimu hizo kuwa ni “kiashiria hatari” cha sera inayoongezeka ya kulenga watu, ikiongeza kwamba waandishi wa habari hawakuwa tena “walengwa tarajiwa,” bali walikuwa “walengwa halisi na wa mara kwa mara.”

Taarifa hiyo imesema utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanya mauaji kwa kuwashambulia waandishi wa habari katika Ukanda wa Gaza katika mwaka huu unaomalizika, akiwemo mwandishi wa habari wa Al Jazeera, Anas al-Sharif, ukiwashutumu baadhi ya waandishi wa habari kwa uongo kuwa wanashirikiana na harakati ya Hamas.

Imeongeza kuwa, licha ya kulaaniwa mara kwa mara na mashirika huru ya vyombo vya habari, utawala huo haujamkamata au kumshtaki yeyote kati ya wanajeshi wake kwa kuwaua waandishi wa habari.

Shirika hilo limesema kuwa mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari yaliongezeka wakati wa vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza vilivyoanza Oktoba 2023, na kuongeza kuwa makumi ya waandishi wa habari wa Kiarabu wameuawa na utawala wa Israel katika miongo miwili iliyopita, akiwemo mwandishi mkongwe wa Al Jazeera, Shireen Abu Akleh, ambaye alipigwa risasi na kuuawa na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi mwaka 2022.

Kamati hiyo imesema utumiaji wa mara kwa mara ya silaha nzito dhidi ya waandishi wa habari ni uhalifu mkubwa wa kivita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *