IRINGA: Bonanza kubwa la michezo lililoandaliwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, lijulikanalo kama Ngajilo Bonanza 2025, limezinduliwa rasmi leo katika Uwanja wa Samora, Manispaa ya Iringa, huku likitarajiwa kuendelea hadi Desemba 31 mwaka huu.

Bonanza hilo linajumuisha michezo zaidi ya 20 tofauti, ikiwemo mpira wa miguu, rede, bao, draft, riadha, masumbwi, kukimbia kwa gunia, mchezo wa vibao, pamoja na michezo ya jadi na burudani kama kula na pete kwa wanawake.

Lengo kuu ni kuibua na kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha afya za wananchi, pamoja na kufungua fursa za ajira na kipato kupitia michezo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, alimpongeza Mbunge wa Iringa Mjini kwa kuanzisha bonanza hilo akieleza kuwa ni jukwaa muhimu la kukuza michezo na kuwatambua vijana wenye vipaji.

Alisema Manispaa na Ofisi ya Mbunge wamekubaliana bonanza hilo liwe linafanyika kila mwisho wa mwaka kama mkakati wa muda mrefu wa kuendeleza michezo.

Ngwada alibainisha kuwa dhamira ya Manispaa ni kuona Iringa Mjini inapata timu imara itakayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania, akisisitiza kuwa bonanza hilo ni hatua ya mwanzo katika safari ya kutimiza azma hiyo.

Aliahidi ushirikiano wa karibu katika hatua za awali za uibukaji wa vipaji na kutoa wito kwa wadau wa michezo, wafanyabiashara na wananchi kushirikiana katika kuendeleza sekta hiyo.

Kwa niaba ya Mbunge wa Iringa Mjini, Katibu wa Mbunge, Yahaya Mpelembwa, aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki na kushuhudia uzinduzi wa bonanza hilo.

Alisema michezo ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya jamii kwa kuwa huimarisha afya, hujenga umoja na mshikamano, na wakati huohuo kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa vijana.

Mpelembwa alieleza kuwa dhamira ya Mbunge Ngajilo ni kuhakikisha vijana wa Iringa Mjini wanapata majukwaa ya kuonesha vipaji vyao, kujitangaza na hatimaye kupata fursa za ajira ndani na nje ya mkoa kupitia michezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *