
Ripoti mpya ya Shirika la Haki za Kimsingi la Umoja wa Ulaya (FRA) ya mwaka wa 2025 imefichua sura isiyo ya kawaida ya kuenea chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya.
Ripoti mpya ya shirika la hilo la FRA inaonesha kwamba ubaguzi wa rangi dhidi ya Waislamu si ubaguzi tena wa mtu mmoja mmoja au hatua za pembeni zisizo na taathira yoyote bali hivi sasa unyanyasaji huo umekuwa ni sehemu ya miundo ya kitaasisi, kisiasa na vyombo vya habari vya Ulaya. Kwa mujibu wa shirika hilo Haki za Kimsingi za wakazi wa bara la Ulaya, hotuba za chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu mwaka wa 2025 zilifikia kiwango cha juu mno kuliko wakati wowote katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya zinaanzia mitaani na kwenye mitandao hadi mahali pa kazi na taasisi za elimu.
Matokeo ya utafiti wa shirika la FRA yanaonesha kwamba, karibu Muislamu mmoja kati ya kila Waislamu wawili wanaoishi katika nchi za Umoja wa Ulaya wamewahi kuripoti kukumbwa moja kwa moja na ubaguzi au udhalilishaji wa rangi na itikadi. Takwimu hizo zimeongezeka kutoka 39% mwaka wa 2016 na kufikia zaidi ya 47% mwaka wa 2025. Wanawake Waislamu wako katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza kazi, kunyanyaswa na kutishiwa usalama wao kwa sababu ya mavazi yao ya Kiislamu. Wakati huo huo, kutokuwa na imani na mifuno ya mahakama na ya ulinzi wa raia kunapelekea waathiriwa wengi kukwepa kuripoti unyanyasaji wanaofanyiwa, suala ambalo linaleta pengo kubwa kati ya takwimu rasmi na ukweli halisi wa mambo.
Huko nchini Uingereza, takwimu za shirika la Tell MAMA zinaonesha kwamba mwaka huu wa 2025 ulikuwa mwaka wenye matukio mengi zaidi ya unyanyasaji dhidi ya Waislamu ikilinganishwa na kipindi cha miaka kumi iliyopita. Unyanyasaji huo unaanzia kwenye mashambulizi ya barabarani na matusi mitandaoni hadi kuharibiwa Misikiti na vitisho kwa wanaharakati wa Kiislamu pamoja na kuenea matamshi ya chuki kwa kiwango kikubwa ambacho kimelilazimisha bunge la Uingereza kuandika upya ufafanuzi rasmi wa maneno “Chuki dhidi ya Uislamu.”
Huko nchini Ufaransa, kuongezeka migogoro ya utambulisho na uhamiaji, pamoja na matukio ya vurugu dhidi ya Waislamu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi kwenye Misikiti na mauaji ya Waislamu, kumezusha tena uhusiano uliopo kati ya sera kali za serikali dhidi ya Waislamu, uhuru wa kila mtu kufuata dini anayotaka na kuongezeka chuki katika jamii ya nchi hiyo dhidi ya Waislamu.
Utafiti wa kitaalamu huko Ufaransa unaonesha kwamba mazungumzo ya kisiasa na vyombo vya habari yana jukumu la moja kwa moja katika ongezeko la kunyanyaswa Waislamu.
Tukiangalia hali ya nchini Ujerumani tutaona haina tofauti na nchi nyingine za Ulaya hasa Uingereza na Ufaransa. Ingawa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani kuna siku ilitangaza kwamba vitendo vya uhalifu wa chuki dhidi ya Uislamu yangelirekodiwa mwaka huu wa 2025, lakini mashirika ya kiraia yanasisitiza kwamba kesi nyingi za unyanyasaji dhidi ya Waislamu haziripotiwi, wala haziorodheshwi katika takwimu rasmi au zinaorodheshwa chini ya anwani nyingine ili kuficha ukweli. Wakati huo huo, sera kali za uhamiaji na mazingira ya baada ya vita vya Ghaza sambamba na msaada wa kisiasa usio na masharti wa viongozi wa Ujerumani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni mambo yaliyoandaa mazingira ambayo yanakwamisha maandamano ya kuliunga mkono taifa la Palestina, hasa yanapobebwa na sauti za Waislamu.
Huko nchini Denmark na Austria pia, matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu pia yamekuwa takriban ni sawa na sera rasmi ya nchi hizo kadri vyama vya mrengo wa kulia vyenye chuki na Uislamu vinavyozidi kupata nguvu.
Kiujumla ni kwamba katika kona zote za Ulaya, Uislamu umeingia kwenye hali nyingine mpya kutokana na vita vya Ghaza na hivi sasa maandamano ya kulaani jinai za Israel huko Ghaza yanaonekana ni uhalifu barani Ulaya. Wanaharakati wengi wa Kiislamu wanashinikizwa mno na wanafuatiliwa na mashirika ya usalama ya nchi za Ulaya huku maandamano ya raia ya kuiunga mkono Palestina yakikandamizwa kwa madai ya kukabiliana na misimamo mikali.
Chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya leo hii si tu ni mgogoro wa kiutamaduni, bali pia ni ishara ya kuporomoka imani ya wapenda haki duniani kwa madai ya kupigania haki yanayopigiwa upatu na madola ya Magharibi. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, sababu ya kuongezeka chuki hizi dhidi ya Waislamu barani Ulaya ni mwamko ulioletwa na vita vya Ghaza, ukubwa wa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na kushindwa madola ya Magharibi kuficha ukweli kuhusu dhati ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel.