SEKTA ya utalii Tanzania imepata ongezeko la asilimia tisa ya idadi ya watalii katika kipindi cha miezi 11 ya kwanza ya mwaka 2025, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.
Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi baada ya kukamilika kwa takwimu za Desemba, kwani msimu wa sikukuu huwa na ongezeko la safari za kimataifa na za ndani ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas alitangaza takwimu hizo jijini Dar es Salaam baada ya kufungua maonesho maalumu ya wanyamapori yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
“Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa kati ya Januari na Novemba 2025, Tanzania imepokea takribani watalii wa kimataifa 173,000 zaidi, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana,” alisema Dk Abbas.
Alisema licha ya changamoto za kiuchumi na kijamii zilizoikumba dunia mwaka 2025, sekta ya utalii nchini
imeendelea kuwa imara na kuvutia idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje ya nchi.
Dk Abbas alikanusha madai yanayosambaa katika mijadala ya umma kuwa idadi ya watalii nchini imepungua, akisisitiza kuwa madai hayo hayana msingi na yanapotosha.
“Kulingana na takwimu hizo, ni dhahiri kuwa sekta ya utalii haijatetereka na inaendelea kufanya vizuri. Tuna imani kuwa pindi takwimu za Desemba zitakapokamilika ifikapo Desemba 31, ongezeko litakuwa kubwa zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa, takwimu hizo zinaungwa mkono na taarifa kutoka taasisi mbalimbali za utalii ambapo kwa mujibu wa TAWA, idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 18, huku utalii wa ndani ukiongezeka kwa asilimia 40 katika vivutio vinavyosimamiwa na mamlaka hiyo.
“Ningeweza kueleza kwa kina kuhusu maeneo mahususi kama Ngorongoro na mengineyo lakini ujumbe wangu mkuu unabaki uleule; Wananchi wasipotoshwe na taarifa zisizo sahihi, wala kuvunjwa moyo na madai yasiyo na ukweli,” alisema.
Maonesho hayo yanafanyika chini ya Kaulimbiu ya “Funga Mwaka Kijanja, Talii” na yalianza Desemba 20, 2025 yakitarajiwa kuhitimishwa Januari 5, 2026.
Akizungumzia maonesho hayo, Dk Abbas alisema ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha utalii katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
“Maonesho haya yanawakutanisha karibu taasisi zote zinazohusika na uhifadhi na utalii ili kuendesha shughuli za uhamasishaji kote nchini. Hapa Dar es Salaam, tunashuhudia tukio kubwa na la kipekee kwa mara ya kwanza,” alisema.
Aliongeza kuwa, maonesho hayo yanajumuisha wanyamapori hai pamoja na maonesho yanayohusiana na uhifadhi, hivyo kuwapatia wageni uzoefu wa kielimu na wa kuvutia.
Dk Abbas aliwahimiza wakazi wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani kutembelea Viwanja vya Sabasaba vilivyopo Barabara ya Kilwa ili kushuhudia wanyama waliopo kwenye maonesho hayo.
“Mimi binafsi nimewaona simba, duma na ngiri (Kasongo). Watu wengi wamekuwa wakisikia tu hadithi za ‘Kasongo’ lakini sasa yupo hapa Sabasaba kwa kila mtu kumuona,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAWA, Mlage Kabange alisema maonesho hayo yamekuwa yakivutia mamia ya wananchi kila siku, wanaokuja kuona wanyama mbalimbali wakiwemo simba, tembo, duma, fisi, nyumbu na ngiri.
Alisema maonesho hayo hufanyika kila siku kuanzia asubuhi hadi jioni, huku viingilio vikiwa nafuu ambapo watu wazima wanalipa Sh 4,000, watoto wenye umri wa zaidi ya miaka mitano Sh 1,000 na watoto walio chini ya miaka mitano wanaingia bure.
