
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ameitaka serikali ya Guinea kukomesha mara moja vitendo vya vitisho na ukiukwaji wa haki za binadamu kabla ya uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika kesho Jumapili tarehe 28 Desemba, akionya kuwa hali ya sasa inahatarisha uhalali wa mchakato wa uchaguzi.
Katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake jijini Geneva Uswisi jana Desemba 26, Türk anasema nafasi ya kiraia na kisiasa nchini Guinea imebanwa sana, huku kukiwa na ripoti za vitisho dhidi ya wanachama wa upinzani, watu kutoweka kwa nguvu kwa misingi inayodhaniwa kuwa ya kisiasa, pamoja na vikwazo vinavyozidi kuongezeka kwa uhuru wa vyombo vya habari.
Visa kadhaa vya watu kutoweka kwa nguvu bado havijapatiwa ufumbuzi, hali inayozua wasiwasi mkubwa miongoni mwa watetezi wa haki za binadamu. Miongoni mwa visa hivyo ni kutoweka kwa ndugu wanne wa msanii na mwanasiasa wa upinzani, Elie Kamano, ambao hawajulikani walipo tangu tarehe 16 Novemba. Hatima na mahali alipo Sanassy Keita, mpiga picha aliyehusishwa na aliyekuwa rais wa zamani Alpha Condé, pia bado haijulikani baada ya kuripotiwa kutekwa nyara na watu wenye silaha na waliovaa kofia mnamo tarehe 27 Novemba.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, muda na hali inayoonekana kuwa ya kulenga watu mahususi ya matukio hayo yameathiri vibaya ushiriki wa kisiasa. Ameonya kuwa vitendo hivyo vinawatisha wanasiasa wa upinzani, vinavuruga kampeni, vinawakatisha tamaa wapiga kura kushiriki, na kuchangia kuenea kwa hali ya hofu miongoni mwa wanasiasa na wananchi kwa ujumla.
Amesema: “Mataukio haya yanahatarisha uhalali wa mchakato wa uchaguzi,” anasema Türk, akisisitiza kuwa uchaguzi huru na wa haki hauwezi kufanyika katika mazingira yenye hofu, shinikizo au ukandamizaji.
Türk amezitaka mamlaka za Guinea kuchunguza kwa haraka na kwa haki madai yote ya watu kutoweka kwa nguvu, kubaini hatima na walipo waliotoweka, na kuhakikisha kuwa wale wote wanaohusika na ukiukwaji wowote wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu. Pia aliitaka serikali kulinda haki za msingi, zikiwemo uhuru wa kujieleza, kukusanyika kwa amani na kushiriki katika siasa, katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.
Guinea imekumbwa na misukosuko ya kisiasa mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni, na waangalizi wa kimataifa wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na uhuru wa kidemokrasia, hususan wakati wa chaguzi.