
Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah nchini Yemen amesema taifa hilo linaendelea kujiandaa usiku na mchana kwa duru ijayo ya vita visivyoweza kuepukika dhidi ya Marekani na Israel, akiahidi kuwa harakati za Muqawama au mapambano ya Kiislamu za Kiyemeni hazitasimamishwa wala kupokonywa silaha.
Sayyid Abdulmalik Badr al-Din al-Houthi, akihutubia kwa njia ya televisheni Ijumaa, alisema: “Tunajiandaa kwa duru ijayo ya mapambano, na tunafanya kazi hii usiku na mchana kwa sababu tunatambua kinachoendelea, tunajua wanacholenga maadui na wanachopanga.”
Kauli zake zimekuja siku moja baada ya Waziri wa Vita wa wa Israel, Israel Katz, kuapa kuendeleza mashambulizi ya kijeshi dhidi ya mataifa kadhaa, ikiwemo Yemen, kufuatia operesheni za nchi hiyo kuunga mkono Palestina.
Al-Houthi alionya kuwa ukimya mbele ya miradi ya kikoloni ya Marekani na Israel utawatia moyo wavamizi kuendeleza dhulma katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu. Alisisitiza haja ya kila mmoja kuwa makini na tayari.
Ameongeza kuwa: “Wamarekani wameshindwa kutuzuia. Kwa silaha zao zote, ndege, mabomu ya angani na baharini, hawakuweza kusimamisha operesheni zetu za kijeshi za kuunga mkono watu wa Palestina, iwe kwa makombora, ndege zisizo na rubani au operesheni za majini.”
Katika hotuba yake, kiongozi huyo wa Ansarullah pia alionya kuhusu njama za Marekani na Israel za kuibua muunda mpya eneo la Asia Magharibui, akitaja kauli za wazi kutoka Washington na Tel Aviv za kutaka “kubadilisha Mashariki ya Kati.” Ametoa wito kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kukabiliana na mipango hiyo badala ya kubaki kimya.
Aliongeza kuwa: “Kuzungumzia kile kinachoitwa Israel Kubwa ni kuwatia watu wa eneo hili chini ya adui mbaya zaidi na dhalimu, na ni janga kwa umma kukubali hilo.”
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amewahi kutangaza hadharani kujitolea kwake kwa ndoto ya “Israel Kubwa” inayojumuisha kupora ardhi yote ya Palestina pamoja na sehemu za Misri, Jordan, Syria, Lebanon, Saudi Arabia na Iraq kwa madai kuwa uporaji wa ardhi hizo “jukumu la kihistoria na la kiroho.”
Akirejelea uhalifu unaoungwa mkono na Magharibi unaofanywa na Israel na Marekani nchini Palestina, Lebanon na Syria, al-Houthi amesema maadui, kupitia “vifaa vyao” katika eneo hili, wanajaribu kuhalalisha mauaji na ukiukaji wa haki.