
Dodoma/Dar. Siku tatu baada ya ajali iliyotokea mkoani Tanga na kusababisha vifo vya watu watano, nyingine imetokea mkoani Dodoma, ambako mmoja amepoteza maisha na wengine 20 kujeruhiwa.
Desemba 25, 2025, saa 10:30 alfajiri, katika Kijiji cha Taula, wilayani Handeni, kwenye barabara kuu ya Chalinze – Segera, mkoani Tanga ilitokea ajali iliyosababisha vifo vya watu watano.
Akizungumzia tukio lingine la ajali, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, Janeth Mayanja, amesema ilitokea saa saba usiku wa kuamkia Desemba 28, 2025 katika Kata ya Haneti, Tarafa ya Itiso, wilayani humo, ikihusisha basi la Super Champion.
“Ni kweli kuna ajali ilitokea katika eneo la Haneti wilayani kwetu, basi la Champion lilikuwa linatoka Moshi kuja Dodoma. Katika ajali hii tumepoteza mtu mmoja mwanamke na wengine wanaendelea na matibabu Hospitali ya Rufaa ya Dodoma,” amesema.
Mayanja amesema mwili wa marehemu bado haujatambuliwa na umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Ernest Ibenzi amekiri kupokea majeruhi 20 na mwili wa mwanamke mmoja aliyekufa katika ajali hiyo.
Dk Ibenzi amesema majeruhi 11 wamesharuhusiwa baada ya kutibiwa lakini tisa wanaendelea na matibabu, huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa hospitalini hapo.
Simulizi ya shuhuda
Arya Mudemu, mmoja kati ya majeruhi wa ajali hiyo amesema ilitokea usiku wa kuamkia leo Desemba 28, 2025.
Amesema walipotoka Moshi mkoani Kilimanjaro, dereva alikuwa akiendesha mwendo wa kawaida lakini baada ya kufika Babati alianza kwenda mwendo wa kasi.
Akizungumza na Mwananchi akiwa wodi namba 16 hospitalini hapo akiendelea na matibabu amesema baadhi ya abiria walipiga kelele wakimtaka dereva apunguze mwendo lakini hakuwasikia.
“Kuna mahali tulipiga kelele sana hata ikalazimika kuongeza sauti lakini hatukusikilizwa,” anasema na kuongeza:
“Kwenye kona mbili zote tulikuwa tunalala upande mmoja, ndipo mbele kidogo tukajikuta tumelala chini wote. Kuna wenzetu walitoka mahututi na wengine walionekana kama wamepoteza maisha.”
Shuhuda huyo wa ajali amesema ilikuwa usiku, hivyo kuwawia ugumu wa kupata msaada.
Hata hivyo, anasema lilipita gari la familia moja lililosimama na kuwapakia majeruhi ambao walipelekwa Hospitali ya St. Gemma iliyopo Miyuji kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Ajali ya Tanga
Ajali iliyotokea wilayani Handeni ilihusisha gari dogo aina ya Toyota RunX, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Moshi, ambalo liligongana na gari la mizigo aina ya Mitsubishi Fuso, lililokuwa likitokea Segera kuelekea Chalinze.
Taarifa ya Jeshi la Polisi ilisema katika ajali hiyo, Justine Jacobo alipoteza maisha na watu wanne walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu ambao nao walifariki dunia wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe.
Waliokufa walitambuliwa kuwa ni Herman Njau, Jerald Manyama, Lightness Lucas na mtoto mdogo Anili Amiri.
Kauli ya Polisi
Hali ikiwa hivyo, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limetangaza kuimarisha doria za usiku na mchana, pamoja na utoaji wa elimu kwa watumiaji wote wa barabara nchini, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuhakikisha usalama kipindi chote cha sikukuu.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 28,2025 Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, William Mkonda amesema askari wako barabarani muda wote wakisimamia sheria na kuwaelimisha madereva na watumiaji wote wa barabara kuhusu wajibu wao wanapokuwa barabarani.
Amesema lengo la juhudi hizo si adhabu pekee, bali kuhakikisha kila mtumiaji wa barabara anafahamu wajibu wake na kuchukua tahadhari zinazostahili ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.
“Hivi sasa mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, hali inayoongeza hatari ya ajali. Tumeendelea kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara kuongeza umakini wanapotumia barabara,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuhimiza utii wa sheria za barabarani bila kusubiri kushurutishwa au kuchukuliwa hatua za kisheria, akisisitiza utii wa hiari ndio msingi wa barabara salama na rafiki kwa kila mtumiaji.
Amewataka watumiaji wa barabara kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo: “Familia yako inakusubiri, zingatia usalama” akieleza inabeba wajibu mkubwa kwa kila mtumiaji wa barabara.
“Kaulimbiu hii inatukumbusha ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi bora ya barabara ili tuwe salama na kuendelea kuwa na furaha sisi pamoja na wapendwa wetu,” amesema.