Kuelekea kikao hicho cha Jumatatu (Disemba 29), mataifa 21 yenye Waislamu wengi duniani yalitowa tamko la pamoja jioni ya Jumamosi (Disemba 27) kuonya dhidi ya “matokeo mabaya sana” kutokana na uamuzi huo wa Israel kwa “amani na usalama kwenye Pembe ya Afrika” na kwenye eneo zima la Bahari ya Shamu.

Somaliland, jimbo la kaskazini mwa Somalia, limekuwa likiendesha mambo yake kama nchi huru kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, ingawa haikuwahi kutambuliwa rasmi na taifa lolote duniani.

Siku ya Ijumaa (Disemba 26), Israel ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuutambua uhuruwa jimbo hilo lililojitenga, hatua iliyolaaniwa hapo hapo vikali na serikali ya Somalia na washirika wake wa kikanda. 

Uamuzi huo wa Israel ulichukuliwa ikiwa ni siku chache tu kabla ya Somalia kuchukuwa wadhifa wa mzunguko wa urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Kwenye tamko hilo la pamoja lililochapishwa na Qatar, mataifa hayo ya 21 yalisema yanaikataa moja kwa moja hatua hiyo ya Israel, wakisema ni “uvunjaji wa wazi wa misingi ya sheria za kimataifa.”

Suala la kuwahamisha Wapalestina lahusishwa

Tamko hilo pia lililaani “majaribio ya kuwaondosha Wapalestina kwa nguvu kutoka kwenye ardhi yao,” baada ya ripoti kwamba utambuaji huo wa Israel kwa Somaliland unahusiana na juhudi za kuwahamisha Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza.

Israel Jerusalem 2025 | Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anasema nchi yake imeitambuwa Somaliland kuwa nchi kamili kwa mujibu wa Makubaliano ya Abraham.Picha: Abir Sultan/Pool/AFP/Getty Images

Mapema mwaka huu, maafisa wa Marekani na Israel waliliambia shirika la habari la The Associated Press kwamba Israel ilikuwa imejaribu kuiomba Somaliland kuwachukuwa Wapalestina kutoka Gaza kama sehemu ya mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani wakati huo wa kuwahamishia wakaazi hao kwenye mataifa mengine. 

Lakini Marekani, ambayo imeshaachana muda mrefu na mpango huo, ilisema siku ya Jumamosi kupitia wizara yake ya mambo ya kigeni kwamba inaendelea “kuyatambuwa mamlaka na uhuru wa Somalia yanayoijumuisha Somaliland.”

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Somaliland, Abdirahman Dahir Adam, alikiambia kituo cha utangazaji cha Israel, Channel 12, siku ya Jumamosi kwamba hatua hiyo haihusiani chochote na mgogoro wa Gaza. 

Kwa mujibu wa ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, utambuaji huo uliwezekana kutokana “na moyo wa Makubaliano ya Abraham”, ambayo yalishuhudia mataifa kadhaa ya Kiarabu kuitambuwa rasmi Israel.

Gazeti la Times of Israel liliripoti kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Moroko, ambazo zote zilijiunga na Makubaliano ya Abraham, hazikuwa miongoni mwa waliosaini tamko hilo la kuikosowa Israel kwa kuitambua Somaliland. 

Somalia, AU, IGAD zalaani 

Siku ya Ijumaa (Disemba 26) serikali ya shirikisho ya Somalia ililaani vikali kile ilichokielezea kuwa ni hatua haramu ya Israel na ikathibitisha kwamba Somaliland inaendelea kuwa sehemu ya mamlaka ya Somalia.

Somalia Hargeisa | mji mkuu wa mkoa wa Somaliland
Sehemu ya mji mkuu wa Somaliland, Hargeisa, ambao ni kituo kikuu cha shughuli za kiuchumi na kisiasa za mkoa huo uliojitenga na Somalia.Picha: Luis Tato/AFP

Taasisi za kikanda barani Afrika nazo pia ziliilaani hatua hiyo ya Israel kuitambua Somaliland, ambapo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, alisema “jaribio lolote la kuyahujumu mamlaka ya Somalia yanaiweka hatarini amani na utangamano barani Afrika.”

Jumuiya ya Ushirikiano ya Pembe ya Afrika (IGAD) ilisema kwenye tamko lake kwamba mamlaka ya Somalia yanatambuliwa kwenye sheria za kimataifa na hatua yoyote kinyume chake ni “kuvunja Mkataba wa Umoja wa Mataifa na makubaliano yaliyoiunda jumuiya hiyo na Umoja wa Afrika.”

Somaliland ilijitangazia uhuru wake kutoka Somalia mwaka 1991 wakati taifa hilo la Pembe ya Afrika lilipoanza kuingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoligeuza kuwa lisilotawalika kwa miaka kadhaa.

Kwa miaka yote hiyo, imekuwa na serikali na sarafu yake yenyewe na imekuwa ikijiendeshea mambo yake kwa kiasi kikubwa bila kuihusisha serikali kuu mjini Mogadishu.

Eneo ilipo Somaliland linatajwa kuwa la kimkakati kwa mataifa yanayowania ushawishi duniani. Mkoa huo wa Somalia upo kwenye Ghuba ya Aden ikiungana na Yemen na Djibouti, ambayo ina vituo vya kijeshi vya Marekani, China, Ufaransa na mataifa mengine kadhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *