Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) zimepanga kufanya mikutano tofauti wiki hii kujadili matokeo ya hatua ya Israel ya kulitambua rasmi eneo la ‘Somaliland, ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili.

Baraza la Arab League leo Jumapili limeitisha kikao cha dharura katika makao makuu ya kikanda ya jumuia hiyo huko Cairo mji mkuu wa Misri kujadili kadhia hiyo. 

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeitisha mkutano huo wa dharura ikiitikia ombi la Mwakilishi wa Kudumu wa Somalia katika jumuiya hiyo kama sehemu ya juhudi za pamoja za nchi za Kiarabu za kushughulikia kile ambacho serikali ya Somalia inasema ni hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa iliyochukuliwa na Israel, inayokiuka wazi mamlaka ya kujitawala ya Somalia na umoja wa ardhi ya nchi hiyo.

Hatua ya Israel ya kuitambua rasmi Somaliland kama nchi huru pia imezidisha wasiwasi kuhusu taathira zake mbaya kwa usalama wa eneo la Pembe ya Afrika na ukanda wa Bahari Nyekundu. 

Lengo la mkutano wa Arab Legue huko Cairo ni kuimarisha msimamo usioyumba wa Waarabu katika kuunga mkono umoja wa ardhi ya Somalia na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo, huku ikipinga hatua zozote za upande mmoja ambazo zinaweza kuhatarisha utulivu wa kikanda.

Baraza la Usalama la UN pia linajiandaa kuitisha mkutano kama huo kesho jioni.

Mkutano huo utafanyika chini ya anwani: “Vitisho kwa amani na usalama wa dunia.”

Ijumaa iliyopita Somalia ilipinga vikali kile ilichoeleza kuwa ni hatua isiyo halali ya Israel kutambua eneo lake lililojitenga, Somaliland, kama taifa huru. Serikali ya Mogadishu imetaja uamuzi huo kuwa ni uvunjaji wa mamlaka na umoja wa ardhi ya taifa.

Umoja wa Afrika (AU) pia umepinga vikali jaribio lolote la kutambua eneo lililojitenga la Somaliland kama taifa huru, ukisisitiza tena dhamira yake thabiti ya kulinda umoja, mamlaka na mipaka ya ardhi ya Somalia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *