ARUSHA: DIWANI wa Viti Maalum Tarafa ya Suye mkoani Arusha, Michelle Mrema, amewataka wanawake nchini kuendelea kuwa walezi wa amani,uvumilivu na mshikamano, akisisitiza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kuwalea watoto watakaokuja kuwa walinzi wa amani ya taifa.
Mrema ametoa rai hiyo wakati wa hafla fupi ya kuwashukuru Wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani Arusha kwa kumuamini na kumchagua kuwatumikia.

Hafla hiyo imefanyika katika Kata ya Sokoni I, Jijini Arusha, ikiwa na kauli mbiu isemayo “Wanawake wa UWT ni msingi wa amani, uongozi na maendeleo ya taifa.”

Amesema ili taifa liendelee kubaki salama, wazazi na walezi wana wajibu wa kuwalea watoto katika misingi ya maadili, uzalendo na mshikamano, itakayowawezesha kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani ya nchi.

Pia ameahidi kushirikiana kwa karibu na wanawake wa UWT katika kutatua changamoto zinazowakabili, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kuleta maendeleo ya kweli.