Nchi za dunia na taasisi mbali mbali za kimataifa zimeendelea kulaani uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kutambua eneo la Somaliland, ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa taarifa ya pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi kadhaa duniani zikiwemo Algeria, Comoro, Djibouti, Misri, Gambia, Iran, Iraq, Jordan, Kuwait, Libya, Maldives, Nigeria, Oman, Pakistan, Palestina, Qatar, Saudi Arabia, Somalia, Sudan, Turkiye, na Yemen, zikilaani kitendo cha utawala wa Kizayuni cha kukiuka wazi mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi ya Somalia.

Taarifa ya pamoja na OIC na nchi hizo imepinga kwa kauli moja hatua ya Israel ya kulitambua eneo la ‘Somaliland’ kama taifa huru, kutokana na athari kubwa za hatua hiyo ‘batili’ kwa amani na usalama katika Pembe ya Afrika, Bahari Nyekundu, na pia athari zake kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa kwa ujumla”.

Mataifa hayo yamekosoa “kukanyagwa kikamilifu na waziwazi kwa sheria za kimataifa” na kutangaza uungaji mkono wao kamili kwa uhuru na mamlaka ya kujitawala Somalia.

Qatar, Iran, Saudi Arabia, Pakistan, China na Nigeria ni miongoni mwa nchi zilizotoa taarfa hapo awali kulaani hatua hiyo ya Israel. Kadhalika Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Harakati ya Kiislamu ya kupigania ukombozi wa Palestina ya Hamas pia zilipinga kitendo hicho cha Wazayuni cha kuitambua Somaliland kama nchi huru.

Aidha Umoja wa Ulaya umesema unaheshimu umoja wa ardhi, uhuru na mamlaka ya kujitawala Somalia, ukitoa mwito wa kufanyika mazungumzo kati ya serikali ya kitaifa ya Somalia na eneo lenye mamlaka ya ndani la Somaliland.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *