
YANGA imetajwa kuwa katika hesabu za kumsajili winga machachari wa Vipers na Uganda The Cranes, Allan Okello anayekiwasha katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 huko Morocco, huku Rais wa klabu hiyo, Hersi Said amekoleza moto akifichua siri za winga huyo.
Injinia Hersi amethibitisha kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa fundi huyo wa mpira anayetumia mguu wa kushoto kutoka Uganda ambaye amekuwa akitajwa kuwindwa na klabu hiyo na nyingine za Tanzania.
Katika mahojiano maalum na kipindi cha ‘Pitch Side kutoka Uganda, Hersi amefichua hayo akisema yeye ni shabiki mkubwa wa wachezaji wazuri kutoka taifa hilo jirani na la Tanzania.
Hersi alisema anampenda sana Okello ambapo amekuwa akimfuatilia kwa muda mrefu staa huyo anayeitumikia Vipers ya Uganda.
Okello kwa sasa yupo Morocco katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika inayoendelea, ambapo juzi Jumamosi katika pambano dhidi ya Tanzania lililoisha kwa sare ya 1-1 alikuwa uwanjani na kukosa penalti muhimu ya dakika za lala salama.
Yanga imekuwa ikielezwa inasaka kiungo mshambuliaji anayecheza nyuma ya straika ambapo hesabu zao Mwanaspoti linafahamu kuwa, zimekwamia kwa Okello.
“Napenda wachezaji wengi wazuri kutoka Uganda ambao ni sehemu ya moyo wangu, nampenda sana Okello, nimekuwa nikimfuatilia kwa muda mrefu sasa tangu anacheza pale Uganda kabla ya kuondoka kwenda kucheza nje na akarudi tena,” alisema Hersi na kuongeza;
“Ngoja nikwambie kitu kaka, nilikuja Uganda 2019 kuangalia vijana wawili kupitia mashindano ya Cecafa, kwanza nilikuja kuangalia beki wa kushoto, Mustafa Kiiza huyu ni mchezaji wa kiwango cha juu sana. Pili nilikuja kumuangalia Okello, ni mmoja ya wachezaji bora na mwingine nampenda ni Bobosi (Byaruhanga) ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana.”
Pia Hersi alifafanua kuwa, Yanga itasajili mchezaji mkubwa kutoka Uganda kama sio dirisha la usajili Januari basi lile kubwa la mwakani.
“Yanga haiwezi kusajili mchezaji mdogo, tuna wajibu mbele ya wanachama na mashabiki wetu tutaleta mchezaji wa kiwango cha juu kutoka Uganda,” alisema Hersi wakati Yanga ikijiandaa kwenda visiwani Zanzibar kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi ikipangwa Kundi C ikiwa na TRA United na KVZ.