
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran ameonya kwamba, kitendo chochote cha uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kitakabiliwa na jibu la haraka na la kuumiza zaidi, akisisitiza utayarifu wa Vikosi vya Jeshi vya nchi hii kukabiliana na maadui na vitisho vyao.
Katika mahojiano na tovuti ya Ofisi ya Uhifadhi na Uchapishaji wa Kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumamosi, Rais Pezeshkian amezungumzia masuala mengi ya kitaifa, pamoja na matamshi na propaganda dhidi ya Iran.
Akijibu swali kuhusu uwezekano wa kufanywa uvamizi mpya na Marekani na Israel dhidi ya Iran, Dakta Pezeshkian amesisitiza kuwa, vikosi vya Jamhuri vya Kiislamu vimejiandaa barabara, kwa upande wa vifaa, silaha na askari, na hivi sasa vina nguvu zaidi kuliko hapo awali kujibu vitendo vyovyote vya uovu.
Aidha ametoa wito tena wa kudumishwa umoja wa kitaifa ili kuzuia uvamizi wa adui na kukabiliana na njama zinazopangwa dhidi ya taifa hili akieleza kuwa, “Ikiwa sisi, wananchi, tutakuwa pamoja na kuungana, [maadui] hao watakatishwa tamaa ya kujaribu kuishambulia nchi yetu.”
Rais wa Iran ameashiria umoja na mshikamano ulioonyeshwa wakati wa vita vya uchokozi vya siku 12 kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Juni, akisema kwamba huduma za kawaida za serikali hazikuvurugwa na ziliendeshwa kama kawaida kwa uratibu, ushirikiano, na mipango ya maafisa na watu.
Pezeshkian amesisitiza kuwa, Marekani, Israel, na Ulaya zinapigana “vita vya pande zote” dhidi ya Iran, akiongeza kuwa nchi hii hivi sasa ina nguvu zaidi, katika uwezo wa kijeshi na nguvu kazi, kuliko ilivyokuwa kabla ya uvamizi wa kijeshi wa Juni mwaka huu.