Dar es Salaam. Si kila mwanaume anafaa kuwa mume, na si kila uhusiano unapaswa kufikishwa katika ndoa.

Wapo wanaume ambao dalili zao huonekana mapema lakini hupuuziwa kwa jina la mapenzi, matumaini au uvumilivu.

Makala haya yanaangazia aina za wanaume ambao mwanamke anapaswa kuwatazama kwa makini kabla ya kuchukua hatua ya kuolewa.

Kuna mwanaume anayejulikana kama “kijana wa mama”. Huyu huishi chini ya kivuli cha mama yake hata akiwa mtu mzima.

Hawezi kufanya uamuzi wowote bila idhini ya mama, hata pale uamuzi huo unapohusu familia yake mwenyewe. Mama huwa ndiye mwenye kauli ya mwisho kuhusu mkae wapi, mfanye nini, mjenge wapi au mtembee wapi.

Kwa mwanaume wa aina hii, mke hubaki kuwa wa pili kila wakati, na ni vyema mwanamke ajue mapema kuwa hawezi kamwe kushindana na mama mkwe katika macho ya mume wake.

Wapo pia wanaume wavivu na wachungu, wanaotaka kunufaika bila kujituma. Aina hii hupenda wanawake wenye uwezo wa kifedha, huku wao wakitegemea kuhudumiwa kila kitu.

Mawasiliano, usafiri, mavazi na hata chakula hugeuzwa kuwa jukumu la mwanamke. Hata mkifika sehemu ya kula au kunywa, mwanaume huyu hula kwa matumaini kwamba mfuko wa mwanamke ndio utalipa. Uhusiano wa namna hii huumiza na hauna mustakabali mzuri.

Aina nyingine ni mwanaume mwenye tabia za “kisanii”. Huyu si msanii kwa taaluma, bali kwa mbinu zake za mapenzi.

Ana uwezo mkubwa wa kuwavutia wanawake wengi kwa wakati mmoja bila wao kujua. Huvaa vizuri, hujiamini kupita kiasi, na mara nyingi hujiona kama zawadi maalum kwa wanawake. Hadithi zake za kusifiwa na kutamaniwa hutumiwa kukuaminisha kuwa wewe ni wa bahati, ilhali ni sehemu ya mchezo wake wa kila siku.

Kuna pia mwanaume asiyepatikana, maarufu kama “Mr Unavailable”. Anaweza kukupa kila kitu cha fedha na mahitaji ya kimwili, lakini hana muda wala uwepo wa kihisia.

Huonekana pale tu anapohitaji mapenzi au ukaribu wa kimwili, na baada ya hapo hupotea. Mara nyingi aina hii hujikuta ikiwahusisha wanawake katika uhusiano wa siri, hata ndoa za watu, jambo linalowaacha wanawake wengi wakiumia na kukosa heshima katika jamii.

Mwanamume lawama

Mwanaume anayekuwa na lawama juu ya maumbile ya mwenza wake naye ni hatari. Huyu hupenda kujilaumu na kukosoa mwili wa mwanamke wake mara kwa mara, iwe ni uzito, umbo au mwonekano. Maneno ya kejeli na dharau hujeruhi sana kihisia, hasa pale ambapo hana nia ya kusaidia kuboresha hali hiyo, bali hulalamika tu. Uhusiano wa aina hii huua kujiamini na furaha ya mwanamke.

Wapo wanaume wasiokubali kukua. Huonekana watu wazima kimwili lakini mawazo na matendo yao bado ni ya kitoto.

Fedha zao hutumika bila mpangilio, muda mwingi huchezea michezo au kuzungukwa na marafiki wasiokuwa na mwelekeo wa maisha.

Mwanaume wa aina hii hushindwa kupanga maendeleo ya baadaye na humchosha mwenza wake haraka.

Mwisho ni mwanaume laini, asiye na uimara wala utayari wa kubeba majukumu. Si suala la uvivu, bali ni kukosa nguvu ya kiuamuzi na kivitendo. Mwonekano na mwenendo wake huashiria kutojiamini na kushindwa kusaidia hata mambo ya kawaida. Kuishi na mtu wa aina hii ni kukata tamaa mapema.

Kwa jumla, mapenzi peke yake hayatoshi kuijenga ndoa imara. Busara, utambuzi wa tabia na uamuzi wa mapema vina mchango mkubwa katika kuepuka maumivu ya baadaye.

Ni vyema mwanamke ajitathmini, ajithamini na awe tayari kuondoka pale dalili zisipoonyesha mustakabali salama wa maisha ya ndoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *