Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Lynn Brown
-
Muda wa kusoma: Dakika 4
Desturi ya kukabidhi pasipoti kwa afisa wa mipaka na kupigwa muhuri unaothibitisha kuwasili katika taifa jipya huenda ikawa historia karibuni.
Mnamo Oktoba 2025, Umoja wa Ulaya ulianza kutekeleza Mfumo wa Kuingia na Kutoka (Entry/Exit System – EES), mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa mipaka unaorekodi taarifa za kibayometria pamoja na tarehe za kuingia na kutoka kwa raia wasiokuwa wa Umoja wa Ulaya wanaosafiri ndani na nje ya eneo la Schengen.
Mfumo huo, unaotarajiwa kutekelezwa kikamilifu Aprili 2026, utachukua nafasi ya kupigwa mihuri ya pasipoti kwa mikono, na badala yake kutumia ukaguzi wa kidijitali, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na usalama katika mipaka ya Ulaya.
Mabadiliko hayo ni sehemu ya mwelekeo mpana wa kimataifa.
Nchi kadhaa, zikiwemo Australia, Japani na Kanada, tayari zinatumia mifumo ya kibayometria katika mipaka yao, huku Marekani ikitangaza mipango ya kupanua matumizi ya teknolojia kama hiyo. Kadiri mifumo ya kidijitali inavyozidi kuenea, huenda ikamaliza taratibu desturi ya muda mrefu ya wasafiri kukusanya mihuri ya pasipoti.
“Matoleo ya awali ya mihuri ya pasipoti yanarudi nyuma hadi Zama za Kati au kipindi cha mwamko-sanaa,” anasema Patrick Bixby, profesa katika Chuo Kikuu cha Arizona State na mwandishi wa License to Travel: A Cultural History of the Passport. “Watawala barani Ulaya walikuwa wakitumia mihuri ya nta kuthibitisha barua za ruhusa za kusafiri. Hapo ndipo chanzo cha desturi hii kilipo.”
Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa nyaraka za kusafiria zimekuwepo kwa karne nyingi, pasipoti za kisasa zilianza kuchukua sura mwanzoni mwa karne ya 20. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, Shirikisho la Mataifa lilisaidia kuweka viwango vya kimataifa vya pasipoti wakati udhibiti wa mipaka ulipoimarishwa.
Kufikia miaka ya 1950, mihuri ya pasipoti ilikuwa imeanza kupewa maana zaidi ya kiutawala, na ikawa ishara ya uhamaji na hadhi wakati dunia ikiingia katika kile kilichoitwa enzi ya dhahabu ya usafiri wa anga.
“Baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kurejea kwa safari za kimataifa, mihuri ya pasipoti ilianza kupata thamani ya kihisia iliyonayo leo,” anaeleza Bixby.
Uwezekano wa kuondolewa kwa mihuri umeibua maoni tofauti miongoni mwa wasafiri.
“Nitakosa mihuri ya pasipoti,” anasema Hristina Nabosnyi, mkazi wa London. “Haikuwa tu uthibitisho wa kuingia nchini, bali pia kumbukumbu za safari na maeneo niliyotembelea.”
Mwandishi wa New York, Elle Bulado, anakubaliana naye. “Ingawa ninaelewa umuhimu wa mifumo ya haraka na yenye ufanisi zaidi, kupokea muhuri kulikuwa ishara ndogo ya kufika mahali ulipokuwa ukiota kulitembelea,” anasema.
Chanzo cha picha, Getty Images
Wengine wanachukua mtazamo wa kivitendo zaidi. Jorge Salas-Guevara, rais na mwanzilishi wa kampuni ya utalii New Paths Expeditions, anaona mabadiliko hayo kama hatua chanya. “Ninasafiri kwa takribani siku 250 hadi 300 kwa mwaka, nikivuka mipaka mara kwa mara. Mfumo huu utanipunguzia muda mwingi.”
Ingawa baadhi ya wasafiri watakosa kumbukumbu za kihisia zinazohusishwa na mihuri ya pasipoti, wengi wanatafuta njia mbadala za kuhifadhi kumbukumbu za safari zao, ikiwemo kukusanya zawadi au vitu vya kumbukumbu.
Kwa mtazamo wa Bixby, hata hivyo, umuhimu wa kuwa na ushahidi halisi wa safari bado unabaki. “Hili ni mjadala mpana kuhusu analojia na dijitali,” anasema. “Kuna kitu cha kipekee kuhusu nyaraka iliyokuwa pamoja nawe ulipokuwepo. Hisia hiyo hupungua pale kila kitu kinapohamishwa kuwa cha kidijitali.”