Bunge la utawala ghasibu wa Israel (Knesset) limelipa idhini baraza la mawaziri la utawala huo kufunga kanali za televisheni za kigeni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa muda wa miaka miwili ijayo, hata katika wakati wa amani bila ya amri ya mahakama.

Bunge la Knesset (bunge la Israel) limeongeza muda wa mamlaka inayoruhusu serikali kufunga chaneli za televisheni za kigeni zinazofanya kazi zake katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Sheria hiyo, ambayo iliidhinishwa na Bunge katika zoezi la upigaji kura lililofanyika usiku kwa kura 22 za ndio na 10 za hapana, imeongeza mamlaka ya muda ya baraza la mawaziri.

Sheria hiyo ilipitishwa wakati wa vita vya Gaza ili kuzima vyombo vya habari vilivyoonekana kuwa tishio kwa usalama wa taifa. Sheria hiyo inaruhusu baraza la mawaziri kukifungia chombo cha habari cha kigeni kwa miaka miwili, hata wakati wa amani, bila kuhitaji amri ya mahakama. Hii ni pamoja na kufunga ofisi za vyombo vya habari, kukamata vifaa vya utangazaji na kuzuia ufikiaji wa tovuti. Sheria hiyo pia inampa waziri wa vita wa Israel mamlaka ya kuchukua hatua za kuzuia matangazo ya satelaiti katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Mamlaka hii, ambayo awali iliitwa “Sheria ya Al Jazeera,” ilitumika kufunga ofisi za kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar na kuzuia matangazo yake mnamo Mei 2024. Hatimaye Al Jazeera ililazimika kufunga ofisi yake ya Ramallah mnamo Septemba 2024. Israel iliishutumu Kanali ya Al Jazeera kwa ubaguzi na upendeleo dhidi ya Israel, na kuunga mkono Hamas katika habari zake. Ukweli wa mambo ni kuwa, walengwa wakuu wa sheria hiyo ni vyombo vya habari vinavyokosoa sera za Israel au kuripoti uhalifu wa utawala huo dhidi ya Wapalestina. Kupitishwa kwa sheria hiyo ili kuzuia vyombo vya habari vya kigeni katika Bunge la Israel kunaonyesha hofu ya utawala wa Kizayuni kuhusu vyombo vya habari huru.

Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel (Knesset)

Hatua hii inaweza kuonekana kama sehemu ya sera ya udhibiti mkali wa taarifa na kukandamiza simulizi pinzani ambazo zinazidi kuhoji uhalali wa utawala huu katika ngazi ya kimataifa. Lengo kuu la utawala wa Kizayuni ni kutumia sheria hii kuangazia tu simulizi zake rasmi za matukio ya kikanda na vita katika vyombo vya habari na kuzuia usambazaji wa maoni pinzani. Bunge la Kizayuni, sambamba na baraza la mawaziri la utawala huo, linaona vyombo vya habari kama tishio kwa usalama wake.

Kwa kutekeleza siasa za mbinyo dhidi ya vyombo vya habari vya kigeni, utawala wa Kizayuni unajaribu kuzuia kutolewa picha na taswira halisi ya hali ya Palestina na uhalifu wa utawala huo kwa fikra za waliowengi duniani. Sheria hii inaonyesha kwamba, utawala wa Kizayuni unaona vyombo vya habari si kama njia ya kupata taarifa, bali kama tishio kwa uwepo kwake. Ukweli wa mambo ni kuwa, vyombo vya habari huru, kwa kufichua ukweli uliopo, ni changamoto kubwa zaidi kwa propaganda za Israel na ngano na simulizi zake za uwongo.

Lililo wazi na bayana ni kwamba, utawala wa Kizayuni unauona ukweli kuwa mmoja wa maadui wake hatari zaidi, kwa sababu unafichua wigo mpana wa uhalifu uliofanywa.

Ni kwa msingio huo ndio maana katika miaka iliyopita utawala bandia wa Israel, umetumia mbinu nyingi kukabiliana na hilo, kubwa zaidi ikiwa ni kushambulia vyombo vya habari ambavyo haviendani na simulizi rasmi za utawala huo na kuzuia shughuli zao katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake.

Uamuzi wa kufunga Al Jazeera na kuwazuia waandishi wa habari wa kigeni kuingia Ukanda wa Gaza ni ushahidi dhahiri wa sera hii na ukiukaji wa wazi wa kanuni na sheria za kimataifa na uhuru wa kujieleza; jambo ambalo sio tu linafichua “uongo wa madai ya Israel kwamba utawala huu ni wa kidemokrasia katika eneo hilo” lakini pia unautambulisha kama adui nambari moja wa vyombo vya habari huru duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *