Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Shamoon Hafez
- Nafasi, BBC Sports
-
Muda wa kusoma: Dakika 4
Pep Guardiola alisema Ijumaa iliyopita kuwa Manchester City lazima waanze kujiandaa kwa maisha bila yeye, akisisitiza kuwa ”hatakuwa kwa klabu hiyo hapo milele”.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 ameacha alama kubwa katika soka la England ndani ya miaka yake tisa Ligi Kuu, akitwaa mataji sita ya ligi pamoja na ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, siku itafika ambapo Guardiola ataamua kuondoka Etihad. Uamuzi huo utaacha pengo kubwa kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki, kwani atakumbukwa kama mmoja wa makocha bora zaidi kuwahi kutokea.
Bado haijulikani ni lini Mhispania huyo ataachia ngazi au kama atamaliza miezi 18 iliyosalia kwenye mkataba wake, lakini taarifa zinaeleza kuwa City tayari wameanza mchakato wa kumtafuta mrithi wake.
Takriban wagombea wawili wametambuliwa, lakini hakuna taarifa rasmi majina yao kamili.
BBC Sport inaangazia majina ya wagombea ambao huenda wakawa mezani kuteuliwa na City endapo Guardiola ataondoka.
Wagombea wa ndani ya Ligi Kuu
Mkurugenzi wa michezo wa City, Hugo Viana, anatarajiwa kuongoza zoezi hilo gumu la kumpata kocha atakayefuata nyayo za Guardiola.
City wanaweza kuanza kwa kuangalia ndani ya Ligi Kuu ambako kuna makocha kadhaa waliothibitisha uwezo wao.
Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, ni miongoni mwa majina yanayotajwa, ingawa alikanusha vikali uvumi unaomuhusisha na City akisema ni tetesi tu.
Maresca amepata mafanikio Stamford Bridge kwa kushinda Kombe la Dunia la Klabu, lakini amekuwa wazi kuhusu kutoridhishwa na uungwaji mkono kutoka kwa uongozi na hitaji la kuongeza uzoefu kwenye kikosi.
Faida kubwa kwake ni uzoefu wa kufanya kazi chini ya Guardiola msimu wa 2022/23 kama kocha msaidizi.
Kwa upande mwingine, Unai Emery ameifanya Aston Villa kuwa tishio la kweli baada ya kuiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja na kuipeleka kwenye ushindani wa Ulaya na ubingwa, wakiwa pointi tatu tu nyuma ya vinara Arsenal.
Andoni Iraola pia anatajwa baada ya kuiongoza Bournemouth kumaliza nafasi ya tisa msimu uliopita, jambo lililowashangaza wengi.
Kocha wa Crystal Palace, Oliver Glasner, yuko nje ya mkataba mwishoni mwa msimu, huku timu yake ikiifunga City kwenye fainali ya Kombe la FA msimu uliopita. Naye Eddie Howe aliimaliza kiu ya Newcastle ya mataji kwa kushinda Kombe la EFL.
Chaguo kutoka Ulaya
Barani Ulaya, City wana chaguo nyingi.
Luis Enrique, aliyewahi kucheza na Guardiola Barcelona, aliipa PSG ubingwa wa Ligi ya Mabingwa msimu uliopita na kutwaa mataji matatu kwa mpigo.
Xabi Alonso aliutikisa Ujerumani kwa kuinyang’anya Bayern Munich ubingwa akiwa Bayer Leverkusen. Ingawa sasa yuko Real Madrid, jina lake bado lina uzito mkubwa.
Vincent Kompany, kocha wa Bayern kwa sasa, angepokelewa kwa mikono miwili na mashabiki wa City. Nahodha wa zamani wa klabu, Kompany alishinda mataji manne ya Ligi Kuu akiwa mchezaji na sasa anaendelea kung’ara kwenye ukocha.
Zinedine Zidane bado hana kazi tangu aondoke Real Madrid, huku Roberto De Zerbi akiendelea kuvutia akiwa Marseille baada ya kipindi kizuri Brighton.
Julian Nagelsmann, licha ya umri mdogo wa miaka 38, anaendelea kuheshimiwa sana, na imeripotiwa kuwa Guardiola anamthamini kwa kiwango kikubwa.
Chaguo la ndani
City pia wanaweza kuangalia ndani ya mfumo wao.
Pep Lijnders, aliyekuwa msaidizi wa Guardiola, ana uzoefu wa ndani ya klabu lakini amekuwa na vipindi visivyofanikiwa alipokuwa kocha mkuu NEC na Red Bull Salzburg mwaka jana.
Aliongoza mechi 51 kwa vilabu hivyo viwili akipata ushindi wa asilimia 47%.Kuingia kama kocha wa City huenda ikawa ni kibarua kigumu kwake.
Kocha wa vijana chini ya miaka 18, Oliver Reiss, naye amefanya kazi kubwa tangu ateuliwe mwaka 2024, akiongoza timu kushinda mechi 21 mfululizo na kutwaa ubingwa wa Premier League North.
Mawazo ya kushangaza
Je, kuna mtu anaweza kuamini hili linaweza kutokea?
Mikel Arteta, aliyewahi kuwa msaidizi wa Guardiola, ameibadilisha Arsenal na kuifanya iwe mpinzani mkubwa wa ubingwa baada ya kumaliza nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo.
Swali ni je, ataivusha Arsenal hadi ubingwa katika msimu huu au City wataendelea kutawala?
Na je, Jurgen Klopp angekubali changamoto hiyo?
Aliyekuwa kocha wa Liverpool alimpa Guardiola ushindani mkubwa zaidi katika Ligi Kuu. Sasa akiwa ndani ya mfumo wa Red Bull, bado haijulikani kama simu kutoka City ingeweza kumbadilisha mawazo.