Somalia imeitaka Israel kubatilisha hatua yake ya kulitambua rasmi eneo la ‘Somaliland, ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili. Somalia imelaani hatua hiyo na kuitaja kuwa kitendo cha “uchokozi ambacho kamwe hakitavumiliwa.

Ali Omar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia ameiambia televisheni ya al Jazeera kwamba serikali itafuata njia zote za kidiplomasia ili kupinga kile ilichokitaja kuwa kitendo cha “uchokozi wa kiserikali” na uingiliaji wa utawala wa Israel katika masuala ya ndani ya Somalia.

Somalia imetoa kauli hiyo kali siku moja baada ya Israel kuwa utawala wa kwanza duniani kuitambua rasmi Somaliland kama taifa huru, hatua iliyolaaniwa na kupingwa pakubwa barani Afrika na mataifa ya Kiarabu. 

Hatua hiyo ya Israel pia imeibua wasiwasi kuhusu iwapo ni sehemu ya mpango unaodaiwa kuwa wa utawala huo ghasibu wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina na kuwapeleka Somaliland

Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 kufuatia vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe lakini haijawahi kutambuliwa rasmi na nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Jamhuri hiyo iliyotangaza kujitenga na Somalia imeanzisha sarafu yake, bendera na bunge, ingawa maeneo yake ya mashariki yameathiriwa na mzozo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia amesema kuwa hatua hiyo ya Israel kamwe haikubaliki na wala haiwezi kuvumiliwa na serikali ya Mogadishu na wananchi walioungana katika kulinda ardhi na kujitawala wa Somalia. 

Itakumbukwa kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilisema siku ya Ijumaa kwamba Tel Aviv imetambua rasmi Somaliland kama “taifa huru na lenye mamlaka kamili” na kusaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *