Sare ya bao 1-1, iliyoipata Taifa Stars juzi katika Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), dhidi ya Uganda ‘The Cranes’, imeiweka timu hiyo katika mtego wa kufuzu hatua ya 16 bora, kwa sababu italazimika kuifunga Tunisia kesho, huku ikiiombea Nigeria ‘Super Eagles’, inayoongoza kundi C, ambayo tayari imeshafuzu iifunge pia Uganda.
Katika kundi hilo la C, Nigeria imefuzu hatua ya 16 bora baada ya kushinda mechi zote mbili ikianza kwa kuifunga Taifa Stars mabao 2-1, kisha kuifunga Tunisia 3-2, huku kwa upande wa kikosi hicho kinachonolewa na Muargentina Miguel Gamondi kikifungwa moja na kutoka sare pia moja hivyo, kuhitaji miujiza ya kufuzu hatua ya 16 bora.
Katika mechi hiyo ya juzi ambayo Stars ilihitaji ushindi ili kuweka matumaini hai baada ya kupoteza kwa Nigeria, ilianza kupata bao la utangulizi la Simon Msuva dakika ya 59 kwa penalti, kisha Uganda kusawazisha dakika ya 80, lililofungwa na Uche Ikpeazu, huku ikikosa pia penalti ya dakika ya 90, ya kiungo mshambuliaji, Allan Okello.
Hesabu kali
Sare hiyo imeiweka Stars katika hesabu ngumu za kufuzu hatua ya 16 bora kutokana na ushindani uliopo, ambapo itahitaji ushindi mechi ijayo dhidi ya Tunisia, huku ikiiombea dua mbaya majirani zetu, Uganda.
Baada ya kupata bao la utangulizi, Kocha, Miguel Gamondi alifanya mabadiliko ya kumtoa Kelvin John na Tarryn Allarakhia huku nafasi zao zikichukuliwa na Dickson Job na Mbwana Samatta, jambo lililosababisha kikosi hicho kubadilika kiuchezaji na kutokana na kucheza kwa kutumia mabeki watatu walioipa Uganda nguvu ya kushambulia zaidi.
Kutumia mabeki wa tatu wa Stars kwa maana ya Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Dickson Job, kulitoa nafasi kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Haji Mnoga kutengeneza balansi nzuri ya kujilinda na wakati huohuo katika kutengeneza mashambulizi, ingawa mbinu hiyo haikufanikiwa kutokana na ubora wa wachezaji wa Uganda.
Kuingia kwa Uche Ikpeazu aliyechukua nafasi ya Jude Ssemugabi na James Bogere baada ya kutoka Travis Mutyaba, kuliongeza nguvu kwa Uganda katika eneo la ushambuliaji hasa kutokana na kasi kubwa ya nyota wa kikosi hicho ambao walikuwa bora kutengeneza mashambuliaji kutokea pembeni, ambako ndiko kulikuwa kunaonekana kuna uimara.
Hata hivyo, uimara wa Stars ulitokana na mabadiliko ya kimfumo wa kutumia mabeki wa tatu ambao husaidia timu kutengeneza balansi nzuri ya kujilinda na wakati huohuo pia wa kushambulia, japo haikuweza kufanya kazi kutokana na uimara wa nyota wa kikosi cha Uganda ambao muda mwingi walikuwa wanatengeneza mashambuliaji kupitia pembeni.
Kuingia kwa Ikpeazu aliyefunga bao la Uganda dakika ya 80, kulitokana na uimara wa nyota wa kikosi hicho hasa kutokana na kutumia vyema mipira mirefu ambayo ilikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Stars, ambao muda mwingi walikuwa wanaulizwa maswali bila ya majibu na kusababisha mechi hiyo kumalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.
Msuva na rekodi
Licha ya Stars kushindwa kutamba mbele ya Uganda na kuweka matumaini hai ya kusoga hatua ya 16 bora ya mashindano hayo, ila nyota wa kikosi hicho, Simon Msuva ameweka rekodi mpya baada ya kufikisha mabao 25 na kufikia rekodi iliyokuwa inashikiliwa na aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, Mrisho Ngassa iliyokuwa imedumu kwa muda mrefu.
Pia, Msuva ameendeleza pia rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyeifungia Taifa Stars bao katika awamu nyingi tofauti za AFCON ambapo hii ni mara ya tatu, baada ya kufanya hivyo mwaka 2019, kule Misri alipofunga dhidi ya Kenya, AFCON ya Ivory Coast mwaka 2023, alipoifunga Zambia na ya mwaka 2025 Morocco alipoifunga Uganda ‘The Cranes’.
Rekodi za AFCON majanga
Wakati Tanzania ikishiriki AFCON ya nne mwaka huu baada ya kuanza kushiriki mwaka 1980, 2019, 2023 na 2025, ila timu hiyo inakabiliwa na rekodi mbovu katika michuano hiyo kwani haijawahi kushinda zaidi ya kutoa sare na kichapo, kwa sababu katika mechi 11 za hatua ya makundi ilizocheza, imepoteza saba, huku nne ikiambulia sare tu.
Ikiwa Stars itashinda kesho dhidi ya Tunisia, itakuwa ni rekodi mpya kwa kikosi hicho katika michuano ya AFCON tangu imeanza kushiriki lakini pia, itakuwa nafasi zaidi kwa timu hiyo kuweka matumaini hai ya kusonga hatua ya 16 bora, kwani itaiombea mema Nigeria ‘Super Eagles’ iliyofuzu tayari itoe sare au ushindi wa aina yoyote ile.