
Dar es Salaam. Tanzania imeendelea kuwa kinara wa mauzo ya bidhaa zake nchini Uganda, ikifikisha thamani ya Dola za Marekani 2.26 bilioni (zaidi ya Sh5.58 trilioni) katika miezi 10 ya kwanza ya mwaka 2025.
Kiasi hicho, kinazidi mauzo ya Kenya na hata jumla ya nchi nyingine zote za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Uganda (BoU), kati ya Januari na Oktoba 2025, Uganda iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 2.26 (zaidi ya Sh5.58 trilioni) kutoka Tanzania, ikilinganishwa na dola bilioni 1.35 (zaidi ya Sh3.33 trilioni) kutoka Kenya.
Hata hivyo, Tanzania iliizidi Kenya katika mauzo ya kila mwezi wa kipindi hicho na hivyo kuthibitisha kuwa Tanzania ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Uganda.
Oktoba pekee, Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 313.25 (zaidi ya Sh773.7 bilioni) kwenda Uganda, zaidi ya mara mbili ya mauzo ya Kenya ambayo ni dola milioni 135.28.
Tofauti hiyo inaonekana zaidi ikilinganishwa na nchi nyingine za ukanda huo wa Afrika Mashariki. Mwaka 2024, Uganda iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 1.87 (zaidi ya Sh4.61 trilioni) kutoka Tanzania, huku Kenya ikisafirisha dola milioni 882.
Sudan Kusini ilichangia dola milioni 37.57, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dola milioni 29.67, Rwanda dola milioni 11.62 na Burundi karibu dola milioni mbili pekee.
Kwa ujumla, Tanzania ilisafirisha bidhaa kwenda Uganda kwa thamani inayozidi jumla ya mauzo ya nchi nyingine zote za Afrika Mashariki.
Hali haikuwa hivyo awali. Mwaka 2020, Kenya na Tanzania zilikuwa karibu kufungana, Uganda ikiagiza bidhaa za dola milioni 808 kutoka Kenya na dola milioni 771.86 kutoka Tanzania.
Kufikia 2022, mauzo ya Tanzania yalishuka hadi dola milioni 281 kutokana na athari za janga la Uviko-19 na changamoto za usafirishaji, wakati Kenya iliendelea na mauzo ya dola milioni 755.5.
Hata hivyo, ndani ya miaka miwili, Tanzania ilirejea, ikiongeza mauzo yake kwenda Uganda kwa zaidi ya dola bilioni 1.6 moja ya marejeo makubwa zaidi ya biashara katika ukanda huo.
Mtazamo wa kiuchumi
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Profesa Haruni Mapesa, amesema faida ya kijiografia na uwekezaji kwenye miundombinu vinaichochea Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na biashara.
“Tanzania ina ufikiaji wa Bahari ya Hindi, bandari za kina kirefu, reli ya kisasa ya SGR, Ukanda wa Kati na mtandao mpana wa barabara. Hii imeifanya kuwa msingi wa uzalishaji unaovutia viwanda vilivyokuwa Asia na Ulaya,” amesema.
Amesema sekta ya elimu inachangia kwa kutoa rasilimali watu wenye ujuzi, huku uwekezaji katika nishati hasa ya umeme wa gesi ukihakikisha upatikanaji wa uhakika kwa viwanda. Hii imekuja wakati muafaka, Uganda ikishuhudia ongezeko la ujenzi na mahitaji ya vifaa vya ujenzi.
Kwa mujibu wa Profesa Mapesa, uimara wa kilimo cha Tanzania pia ni nguzo muhimu.
“Uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara bado uko imara licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Hili linaipa Tanzania faida kama msambazaji wa chakula na kituo cha kuchakata mazao,” amesema.
Kwa mchanganyiko wa jiografia, miundombinu, ujuzi na kilimo, Tanzania inaendelea kujijenga kama kitovu cha uzalishaji na usambazaji kwa Afrika Mashariki, SADC na soko pana la Afrika kwa mujibu wa Profesa Mapesa.