
Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine hana mpango wowote hadi yeye Trump aidhinishe.
Zelensky amedai kuwa ametayarisha mpango mpya wa amani wenye vipengee 20 kwa ajili ya kuhitimisha vita vya Ukraine. Rais wa Ukraine atauwalisha mpango huo wa amani kwa Trump katika mkutano wa leo Jumapili huko Florida, Marekani.
Hata hivyo Trump amesema katika mahojiano na gazeti la Politico kwamba Rais wa Ukraine hana mpango wowote wa amani. “Hana chochote hadi nitakapoidhinisha mimi,” Trump ameliambia Politico katika mahojiano ya Ijumaa na kuongeza: Tusuburi tuone Zelensky ana nini.”
Trump amesema kuwa anataraji kuzungumza na kiongozi wa Russia hivi karibuni.
Fremu ya mpango mpya wa amani wa Zelensky inajumuisha eneo lililopendekezwa lisilo la kijeshi katika hali ambayo mazungumzo kati yake na Trump yanatazamiwa kujadili dhamana ya Marekani kwa usalama Ukraine.
Mpango huo wa amani wa Rais Zelensky wa Ukraine ambao umeelezwa na maafisa wa wa Kyev kuwa jaribio lenye lengo la kulegeza kamba bila kuachia ardhi yoyote, umekaribishwa kwa ubaridi mjini Washington.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, kwa mujibu wa mpango wa vipengee 20 uliopendekezwa na Trump, eneo la Donbas linalozungumza lugha ya Kirusi huko mashariki mwa Ukraine litajiunga na Russia. Rais wa Marekani amekuwa akimshinikiza Rais wa Ukraine akubali mpango huo ili kuhitimisha vita na Russia.