Mbarali. Ni saa nne asubuhi katika Kijiji cha Mwatenga, Kata ya Mahongole wilayani Mbarali. Jua bado halijawa kali, lakini wakulima tayari wako mashambani na kando ya mashamba hayo maji yanatiririka kwa utulivu kwenye mkondo uliokuwa umepotea kwa miaka katika Mto Mlowo.

Kwa wakazi wa eneo hilo wanasema kurejea kwa mto huo si tukio la kawaida ni hadithi ya matumaini mapya baada ya kipindi kirefu cha kukosa maji, mazao kukauka na maisha kuyumba.

“Zamani tulilima kwa mazoea tu hatukuwa na uhakika wa maji,” anasimulia Hamis Mwatenga, mkazi wa kijiji hicho huku akiendelea kusema

“Lakini sasa maji yanaonekana, na matumaini ya mavuno yamerudi,”

Kwa muda mrefu, mito mingi katika Bonde la Usangu ilikuwa imejaa mchanga na kupoteza uelekeo wake wa asili kutokana na mmomonyoko wa ardhi na shughuli za kibinadamu na athari zake ni kilimo kudorora, mifugo kukosa maji na migogoro ya matumizi ya rasilimali hiyo muhimu kuongezeka.

Hali hiyo ndiyo iliyochochea kuanzishwa kwa Mradi wa NBS–USANGU unaotekelezwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Serikali ya Japan, ukiwa na lengo la kurejesha ikolojia ya mito kwa kutumia suluhisho la asili (Nature-Based Solutions).

Akieleza malengo ya mradi huo Leo Desemba 27, 2025 wakati akizungumza na Mwananchi Digital Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Mhandisi David Munkyala, anasema urejeshaji wa mito ni hatua muhimu katika kulinda rasilimali za maji na kuhakikisha zinawanufaisha wananchi kwa muda mrefu.

“Kwa miaka mingi, mito ya Usangu ilipoteza mikondo yake ya asili na kupitia mradi huu, tunairudisha ili maji yarudi mahali yalipokusudiwa na yatumike kwa tija,” anasema Munkyala .

Kwa mujibu wa Mhandisi Munkyala, urejeshaji wa Mto Mlowo utaongeza upatikanaji wa maji kwa kilimo na mifugo, sambamba na kupunguza migogoro iliyokuwa ikitokana na matumizi holela ya maji.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa NBS–USANGU, David Muginya, anasema mradi huo unaathiri moja kwa moja maisha ya wananchi kwa kuimarisha uzalishaji wa kilimo, usalama wa chakula na kipato cha kaya.

“Urejeshaji wa mito ni zaidi ya mradi wa mazingira ni uwekezaji wa moja kwa moja katika maisha ya wananchi,” anasema Muginya, akiongeza kuwa tayari vijiji kadhaa vinavyopakana na mito hiyo vimeanza kushuhudia mabadiliko chanya.

Wananchi nao wameanza kubadili mtazamo wao kuhusu uhifadhi wa mazingira ambapo Omary Makolo, mkazi wa Kijiji cha Ilaji, anasema mradi huo umeongeza uelewa wa umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji.

“Tumejifunza kuwa tusipolinda mito yetu, hatutakuwa na maisha. Sasa tunashiriki katika uhifadhi,” anasema Makolo.

Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa Mradi wa NBS–USANGU waliotembelea eneo hilo, akiwemo Said Juma na Simon Kitereja, wanasema urejeshaji wa Mto Mlowo ni ushahidi wa matumizi sahihi ya fedha za mradi na dhamira ya dhati ya kulinda rasilimali za maji.

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa mafanikio ya mradi huo yatategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wananchi katika kulinda maeneo yaliyorejeshwa.

Kwa wananchi wa Usangu, kurejea kwa mito ni zaidi ya mafanikio ya kitaalamu na ni kurejea kwa uhai wa ardhi yao, uhakika wa chakula na matumaini ya kesho iliyo bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *