Unywaji wa pombe unasababisha vifo vya watu zaidi ya 800,000 kila mwaka barani Ulaya, na kusababisha kifo kimoja kati ya kila vifo kumi na moja, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Katika ripoti mpya iliyochapishwa wiki hii, shirika hilo limesema bara hilo lina “viwango vya juu zaidi vya unywaji pombe duniani,” huku ulevi ukichangia kwa kiasi kikubwa vifo vya mapema na majeraha. Ripoti hiyo imesema kuwa, kategoria kubwa zaidi za vifo hivyo vilitokana na kujidhuru, majeraha ya ajali za barabarani na kuanguka.

Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataiga, unywaji wa pombe pia umehusishwa kwa karibu na vurugu na mivutano miongoni mwa watu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi na unyanyasaji wa majumbani, na kubaini kuwa ni sababu kubwa inayochangia vifo vya majeraha ya vurugu katika eneo lote la Ulaya.

Utafiti wa WHO umebainisha kuwa, vijana wanakabiliwa na hatari maalum, huku pombe ikiathiri ukuaji wa ubongo na kufanya maamuzi wakati wa ujana na kwenye utu uzima.

Carina Ferreira-Borges, Mshauri wa Kanda wa Pombe, Mihadarati na Afya ya Magereza katika shirika la WHO barani Ulaya amesema: Pombe ni kiungo chenye sumu ambayo sio tu husababisha aina saba za saratani na magonjwa mengine yasiyoambukiza, lakini pia hudhoofisha uamuzi na kujidhibiti, hupunguza muda wa athari, hupunguza uratibu, na kukuza tabia ya kuchukua maamuzi hatari.” 

Huku hayo yakiarifiwa, matokeo ya utafiti uliofanywa nchini Marekani hivi karibuni yanaonyesha kuwa, unywaji wa pombe kupita kiasi unasababisha kifo cha mtu mmoja kati ya kila watano wanaofariki nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *